Yanga: Tutawashangaza Caf

10Oct 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Yanga: Tutawashangaza Caf
  • ***Nahodha, Zahera wamwaga cheche droo ya mechi ya mchujo ikipangwa huku wakijigamba...

TUTAWASHANGAZA! Nahodha msaidizi wa Yanga, Juma Abdul, amesema wamejipanga kupeperusha vema bendera ya Tanzania kuelekea katika hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Nahodha msaidizi wa Yanga, Juma Abdul

Yanga, ambao ndio wawakilishi pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano hayo ya kimataifa, walitarajia kuwafahamu wapinzani wao jana usiku, baada ya kufanyika kwa droo ya michuano hiyo huko jijini Cairo, Misri.

Akizungumza na gazeti hili jana, Abdul, alisema wanafahamu mechi zote za hatua hiyo ya makundi ni ngumu na zenye ushindani, lakini wamejiandaa kupambana ili kuhakikisha wanasonga mbele.

Abdul alisema wanafahamu wanapofanya vizuri, wanajiweka katika nafasi ya "kuvuna" fedha za Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambazo wakizipata, zitawasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali klabuni kwao.

"Tunaweza kufika mbali na tukawashangaza wengi, katika mpira lolote linaweza kutokea, tunajua ni hatua ngumu, lakini kama tukiwa makini, tuna nafasi ya kusonga mbele, kikubwa ni kuendelea kujipanga," alisema beki huyo ambaye amerejea katika kikosi cha kwanza.

Naye Kocha Mkuu wa Yanga Mkongomani Mwinyi Zahera, amesema kuwa anaendelea kurekebisha mapungufu aliyoyaona katika mechi zilizopita ili waweze kupata matokeo mazuri katika mashindano hayo ya kimataifa na mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Bado timu haichegi vizuri, tulianza ligi kwa kupoteza, tukapata pointi moja, na tukaifunga Coastal Union, bado tunahitaji kuwa imara ili kukabiliana na ushindani, tunaelekea sehemu ngumu zaidi, katika Ligi ya Tanzania na Kombe la Shirikisho Afrika," Zahera alisema.

Aliongeza kuwa anaamini wachezaji wake ambao ni majeruhi, watakuwa wamepona na kuanza kuitumikia timu baada ya mechi za ligi zitakapoanza tena.

Yanga ambayo iliong'olewa na Zesco katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ina jumla ya pointi nne baada ya kucheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara huku watani zao Simba wenye pointi 12 kileleni mwa ligi hiyo, wakiwa wameshuka dimbani mara nne.

Habari Kubwa