Simba kufuata kisu cha Azam Jumapili

10Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba kufuata kisu cha Azam Jumapili

KIKOSI cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam Jumapili kuelekea Kigoma kwa ajili ya kusaka makali kwenye mechi mbili za kirafiki ili kujiimarisha kabla ya kukutana na Azam FC baadaye mwezi huu, imeelezwa.

Hata hivyo, kabla ya kwenda Kigoma, Simba inatarajia kucheza mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Bandari FC kutoka Kenya, ambayo itachezwa keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema wanatarajia kwenda Kigoma na wachezaji wote waliobaki kikosini na lengo ni kuwapa nafasi mashabiki wao wa mkoa huo na jirani kuiona timu yao.

Rweyemamu alisema mbali na faida za kiufundi, ziara za mikoani zimekuwa zikiwajenga wachezaji wao na kufahamu thamani halisi ya klabu wanayoitumikia.

"Tutaondoka Jumapili, tukiwa huko kama ilivyo desturi, tunatarajia kushiriki katika shughuli za kijamii ambazo zitakuwa zimeandaliwa," alisema Rweyemamu.

Ikiwa Kigoma, Simba inatarajia kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Mashujaa utakaopigwa Jumatatu Oktoba 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma na baada ya siku mbili itakutana na Aigle Noir ya Burundi kwenye uwanja huo huo.

Baada ya mechi hizo za kirafiki, Simba itarejea jijini kuwasubiri Azam FC kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Oktoba 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.

Habari Kubwa