Hakimu kuburuzwa mahakamani tuhuma za rushwa

10Oct 2019
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Hakimu kuburuzwa mahakamani tuhuma za rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Shinyanga, inatarajia kumfikisha mahakamani Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Benjamini Mhangwa, kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh. 200,000.

Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Husseni Mussa

Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Husseni Mussa, alisema juzi kuwa Septemba, mwaka huu, hakimu huyo aliomba rushwa ya Sh. 300,000 kutoka kwa mzazi ambaye mtoto wake alibakwa, ili amsaidie kushinda kesi yake na kufanikiwa kukamatishwa na Sh. 200,000. 

Alisema hakimu huyo alimfuata mzazi wa mtoto ambaye amebakwa na kumrubuni kuwa ametumwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kishapu, Wilberforce Luhwago, ili wamsaidie kupata ushindi kwenye kesi hiyo.

"Baada ya mzazi huyo kuombwa kiasi hicho cha fedha alitoa taarifa kwetu na  tukamwekea mtego hakimu wa Sh. 200,000 na kufanikiwa kumkamata na fedha hizo kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007," alisema Mussa.

"Katika uchunguzi ambao tumeufanya, tumebaini kuwa fedha hizo za rushwa hazikuombwa na Hakimu Luhwago bali ziliombwa na hakimu huyo wa Mahakama ya Mwanzo tutakayemfikisha mahakamani," aliongeza.

Mussa alitoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa taarifa kwa taasisi hiyo juu ya vitendo vya rushwa ili wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria  na kukomesha vitendo hivyo.

Habari Kubwa