Aliyepinga kufukuzwa kazi TRA kwa cheti cha kughushi ashindwa kesi

10Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Aliyepinga kufukuzwa kazi TRA kwa cheti cha kughushi ashindwa kesi

TUME ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), imesema uamuzi uliofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dhidi ya mlalamikaji Salehe Hussein wa kufukuzwa kazi baada ya kukutwa na cheti cha kughushi cha kidato cha nne, ulikuwa sahihi.

Akisoma hukumu ya kesi hiyo Jumatatu jijini Dar es Salaam, Ofisa Mfawidhi Mkoa wa Dar es Salaam, Usekelege Mpulla, alisema TRA walifuata utaratibu wa kumwachisha kazi mlalamikaji (Hussein) aliyekuwa Ofisa wa Msaidizi wa kushughulikia ulinzi wa mipaka.

Kesi hiyo ilikuwa ikisimamiwa na wakili wa upande wa mlalamikaji Heriel Munisi na upande wa mlalamikiwa, Jacqueline Chunga.

Upande wa mlalamikiwa ulikuwa na mashahidi wawili, Ofisa Rasilimali Watu wa TRA, Sixmund Matembo na Ofisa Rasilimali Watu TRA kituo cha Zanzibar, Haula Issa.Upande wa mlalamikaji ulisema hauna shahidi mwingine.

Mpulla alisema kuwa Chunga alieleza kuwa cheti kilichohakikiwa na kuonekana ni cha kughushi kilikuwa na namba P.0083-390 cha mwaka 1990 chenye jina la Salehe Hussein Salehe na kwamba kilikutwa kwenye jalada binafsi la mlalamikaji.

"Kabla ya kutoa amri za mwisho nawiwa kuvaa vazi la kuelimisha na kusema maneno mawili kuhusiana na kile nilichobainika kwenye shauri hili ambalo nalichukulia ni la kipekee," Mpulla alisema.Alisema inasikitisha kuona mtu anaajiriwa bila vyeti vyake kuhakikiwa vyema hali inayosababisha kuwapo kwa vyeti vya kughushi kutokana na mbegu iliyopandwa na waajiri wenyewe.

"Ifahamike kwamba kwa wengi waaminio, hakuna kitu kinachodumu isipokuwa Mungu hivyo ukiukwaji wowote wa sheria, kanuni na taratibu hata kama mwanzo hautaonekana inakuwa ni mbegu ambayo haijalishi imekaa muda gani, siku moja inaweza kuota na kuleta matunda ambayo yeyote aliyepanda atavuna.

"Labda, nimeandika kwa namna ambayo inaweza kutafsiriwa kama vidonge vichungu ambavyo ni vigumu kumeza japokuwa vinatarajiwa kwamba somo kubwa kama nchi tumejifunza."

Alisema mbali na Tume kufikia hitimisho kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa, mlalamikiwa hawezi kukwepa lawama katika zoezi hilo pamoja na waajiri wengine nchini.

"Ninaona ni busara kuwakumbusha waajiri wote ikiwamo serikali kuzingatia sheria na miongozo katika mazoezi ya kuajiri watu," alisema.

Akielezea ushauri huo, Mpulla alisema kuachishwa kazi kwa mlalamikaji kulikuwa halali.

Alimuru kuwa mgogoro pamoja na madai yote yametupiliwa mbali na kila upande ubebe gharama zake.Pia alisema ndani ya wiki sita mlalamikaji kama atakuwa hajaridhishwa na hukumu iliyotolewa na Tume hiyo, anaweza kukata rufani ili kiu ya wengine wengi ambao wanaamini zoezi hilo halikuwa la haki na wengine kuamini lilifanyika kwa haki, wapate tafsiri yake.

"Mimi siyo Mungu nimetimiza wajibu wangu wa kutafsiri nilivyoona inafaa kwa yale mliyoyaleta kwangu, ninawashauri ndani ya wiki sita muende Mahakama Kuu ya Tanzania mkaangalie hukumu hii niliyoitoa na yenyewe iwe na ya kwake, na hata ikihukumiwa vinginevyo huko bado ninashauri muende Mahakama ya Rufani ambayo ndiyo yenye maamuzi ya mwisho," alisema.

Awali, akisoma ushahidi uliotolewa kwenye shauri hilo alisema shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, alikiri kumtambua mlalamikaji tangu 1996 na kabla ya kuhamia kwenye mamlaka hiyo, alitokea Wizara ya Fedha.

Katika ushahidi wake, aliieleza Tume hiyo kuwa mlalamikaji alianza kazi rasmi mwaka 1997 na kufukuzwa mwezi Novemba mwaka 2018.

Shahidi wa pili, Issa alieleza kuwa anamjua malalamikaji kama mmoja wa waliokuwa waajiriwa TRA katika nafasi ya Ofisa wa Msaidizi aliyekuwa akishughulikia ulinzi wa mipaka.

Katika ushahidi wake aliieleza Tume hiyo kuwa, alipokea maelekezo kutoka Makao Makuu TRA kuhusu operesheni ya vyeti vilivyoghushiwa na kwamba wafanyakazi wote walipewa taarifa na kutakiwa kuviwasilisha vyeti halisi.

Habari Kubwa