Chanjo ya mifugo sasa lazima

10Oct 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Chanjo ya mifugo sasa lazima

CHANJO kwa mifugo sasa ni lazima na siyo hiari, baada ya serikali kuboresha mwongozo wa matumizi na udhibiti wa dawa za majosho wa mwaka 2019 kwa lengo la kudhibiti magonjwa yatokayo na wanyama kwenda kwa binadamu.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega

Katika kutekeleza hilo, tayari serikali imeshanunua lita 11,000 za dawa za kudhibiti magonjwa yatokanayo na wanyama kwa lengo la kuongeza ubora wa vyakula vitokanavyo na mifugo.

Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, wakati akifungua mdahalo wa vyakula vya asili ya wanyama na mchango wake katika masuala ya afya ya umma na lishe katika kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani mwaka huu.

Katika mdahalo huo, uliohusisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba Muhimbili (Muhas), pia alizindua mikakati ya kitaifa ya kuzuia na kudhibiti magonjwa ya brusela na kimeta kwa binadamu na wanyama.

"Chanjo sasa ni lazima siyo hiari, kila mfugaji ana wajibu wa kutoa chanjo kwa mifugo yake ili kupunguza magonjwa na ambao hawatafanya hivyo, atawajibishwa kwa mujibu wa sheria na adhabu ni kutumikia kifungo, kulipa faini au yote mawili,” Ulega alisema.

"Ina maana kama jamii itatumia nyama, mayai na maziwa kama inavyotakiwa, itakuwa na afya njema, hivyo kuipunguzia Wizara ya Afya mzigo wa bajeti wa Sh. bilioni 200 inayotengewa kwa mwaka kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba kwa ajili ya wagonjwa," Ulega alisema.

Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) nchini, Fred Kafeero, alisema wameendelea kujenga uwezo wa utayari wa kukabiliana na kuitikia milipuko ya magonjwa kwa kutumia utaratibu wa afya moja.

Alisema unawapatia watu protini ambayo ni sehemu muhimu katika chakula kwa sababu asilimia 50 ya idadi ya watu wanategemea wanyama moja kwa moja kama chanzo cha chakula chao na kiwango kingine kikubwa pia hutegemea hivyo ingawa siyo moja kwa moja.

"Uzalishaji wa tija kwa mazao ya mifugo ni suala muhimu linalohusu maisha ya watu. Kwa miaka mingi FAO imekuwa ikijihusisha na uimarishaji wa uwezo wa kitaifa wa kuzuia, kugundua na kudhibiti magonjwa ya wanyama nchini," Kafeero alisema.

Habari Kubwa