Kasike: Simamieni wafungwa kutatua uhaba makazi askari

10Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
SONGWE 
Nipashe
Kasike: Simamieni wafungwa kutatua uhaba makazi askari

KAMISHNA Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike, amewataka wakuu wa magereza Tanzania Bara kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo agizo la Rais John Magufuli kuhusu ujenzi wa nyumba za makazi ya askari wa jeshi hilo nchini kwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa waliopo magerezani.

Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike

Akizungumza mkoani Songwe baada ya kukagua miradi ya ufyatuaji wa matofali ya kuchoma na ujenzi wa nyumba za maofisa na askari katika Magereza ya Ileje, Mbozi, Ngwala na Kambi ya Mkwajuni, Kasike alisema ujenzi wa makazi ya askari unaoendelea katika vituo mbalimbali nchini ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli katika kutatua changamoto ya makazi kwa watumishi wa jeshi hilo.

 "Mkakati wa utatuaji wa changamoto ya uhaba wa nyumba za maofisa na askari lazima utiliwe mkazo na kupewa kipaumbele katika kuwatumia wafungwa  waliopo magerezani katika suala la ujenzi sambamba na uzalishaji wa chakula cha kutosha ili kuipunguzia serikali gharama za kuwahudumia wahalifu wote walipo magerezani,” alisema Kasike.

Katika hatua nyingine, Kasike aliupongeza uongozi wa Wilaya ya Songwe kwa kuanzisha ujenzi wa gereza jipya katika mji wa Mkwajuni ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Songwe.Alisema uwapo wa gereza hilo katika Wilaya ya Songwe utasaidia katika kumaliza tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye Gereza la Wilaya ya Mbozi.

“Kutokuwapo kwa magereza ya wilaya kunasababisha msongamano wa wafungwa na mahabusu katika magereza ya jirani, pamoja na kuchelewesha upatikanaji wa haki, hivyo nimpongeze sana Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Opulukwa  na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama kwa kuwezesha kuanza kwa ujenzi wa gereza. Kimsingi, utatatua tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Gereza la Mbozi,” alisema.Naye Opulukwa alishukuru ujio wa Kamishna Jenerali katika ziara yake ya kikazi katika Gereza la Ngwala pamoja na Kambi ya Mkwajuni ili kujionea hali halisi ya uendeshaji wa jeshi hilo, wilayani Songwe.

Habari Kubwa