TRA yapewa siku 60 kuwasilisha walipakodi

10Oct 2019
Benny Mwaipaja
Nipashe
TRA yapewa siku 60 kuwasilisha walipakodi

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, ameipa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA miezi miwili na nusu kuandaa na kuwasilisha wizarani orodha ya walipakodi, idadi ya majengo na mabango yote yaliyoko katika Mkoa wa Dar es Salaam ili kupata takwimu sahihi za idadi ya walipakodi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji

Dk. Kijaji ametoa muda huo hadi ifikapo Desemba 31, mwaka huu. 

Alitoa muda huo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kikazi katika Mamlaka hiyo, mkoa wa kikodi wa Temeke ili kukagua utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hayo kwa lengo la kubaini fursa na changamoto za masuala ya ukusanyaji kodi.

Alisema pamoja na mamlaka hiyo kufanya vizuri katika makusanyo ya mapato mwezi Septemba 2019 kwa kukusanya Sh. trilioni 1.78, kiasi hicho bado ni kidogo ikilinganishwa na mwamko wa wananchi uliopo hivi sasa wa kulipa kodi.

Aliitaka TRA kuwasilisha kwake takwimu ya ongezeko la walipa kodi lililotokana na ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali nchini, akisema lengo la Rais Dk. John Magufuli kugawa vitambulisho hivyo lilikuwa ni kuongeza wigo wa walipa kodi watakao kuwa wanafuzu kwa kuongeza mitaji yao, hivyo ni vyema kujua idadi yao na mahali walipo.

Kwa upande wa kodi ya majengo, Dk. Kijaji aliitaka TRA kuhakikisha inapata orodha ya nyumba zote nchini kwa kuorodhesha wamiliki wa nyumba hizo na mawasiliano yao na kisha kuandaa kanzidata itakayosaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi hiyo. 

"Nataka pia mkague watumiaji wote wa mashine za utoaji risiti za kielektroniki (EFD) kwa wafanyabiashara wa Temeke ili kuhakikisha kila anayeuza anatoa risiti na anayenunua anadai risiti na kwa kufanya hivyo itasaidia  kuongeza makusanyo ili taifa liendelee kujitegemea kimapato," alisisitiza Dk. Kijaji. 

Awali akimkaribisha Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Meneja wa TRA, mkoa wa kikodi wa Temeke, Paul Walalaze, alisema mkoa wake una idadi ya walipakodi 437,539 na kwamba katika mwaka 2018/19, ulipanga kukusanya Sh. bilioni 395 na kufanikiwa kukusanya Sh. bilioni 328.5 sawa na asilimia 85 ya lengo.

"Tumekusanya pia kodi ya majengo Sh. bilioni 1.4 kati ya malengo ya kukusanya Sh. bilioni 1.6, kodi ya mabango Sh. bilioni 2.2 kati ya lengo la kukusanya Sh. bilioni 2.3 sawa na mafanikio ya asilimia kati ya 87 na asilimia 95," alisema Walalaze.

Ofisa Mwandamizi Mkuu wa TRA, Hamisi Lupenja, alimhakikishia Dk. Kijaji kuwa watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ili kuboresha ukusanyaji mapato ya serikali ikiwamo kutoa elimu kwa walipakodi.

Habari Kubwa