Waumini watwangana makonde kanisani

10Oct 2019
Peter Mkwavila
DODOMA
Nipashe
Waumini watwangana makonde kanisani

WAUMINI wa Kanisa la Assemblies of God (TAG) Swaswa Mnarani mjini hapa, wametwangana makonde baada ya mchungaji wa kanisa hilo, Msafiri Malendaa, kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuuza viwanja 10 vya kanisa hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi

Tukio hili lilitokea Oktoba 6, mwaka huu, majira ya saa nne asubuhi ndani ya kanisa hilo.Nipashe ilishuhudia mchungaji Malendaa akikamatwa na polisi wakati akiendesha ibada madhabahuni na kupandishwa kwenye gari la polisi namba PT 4300.

Tukio hilo lilisababisha waumini kutoka nje ya kanisa na kuanza kuvutana huku wengine wakimtuhumu mchungaji huyo kuwa ni mwizi, huku wengine wakimtetea hali iliyosababisha baadhi yao kuanza kupigana makonde.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa waumini hao, Lidya Mgowela, alisema anashangaa kuona katibu wa kanisa akipigana na muumini.

"Nimetoa sadaka yangu, nilivyomaliza nikaona watu wanaanza kupigana nikaogopa sana nimekuja kutubu halafu kuna mambo haya, nipo hapa nje naangalia kinachoendelea ila ni mbaya sana mimi sijui chochote, nimeumia tena kanisa lenyewe ni kiroho," alisema.

Naye Paul Mathew alisema Jiji la Dodoma lilibomoa kanisa hilo katika eneo la Swaswa Mnarani kwa ajili ya kupisha ujenzi wa barabara na kulilipa kifuta jasho kanisa viwanja 10 katika eneo la Ilazo Extension ili viuzwe na lijengwe kanisa jipya.

Alifafanua kuwa Jiji lilitoa viwanja hivyo na kumpa mchungaji huyo ambaye ilidaiwa aliandika viwanja hivyo majina ya familia yake na ndugu, jamaa na marafiki ili iwe rahisi kuviuza.

"Tuliona ni sawa kwani alisema vikiandikwa jina la taasisi vitakuwa vigumu kuuzwa na kanisa lilipewa kiwanja kingine cha kujenga hivyo kama tungeviuza vile tungepata fedha za kuendelea na ujenzi.

"Lakini alipoviuza fedha hakuna na hatujui kinachoendelea ukimuuliza anakufukuza kanisani, hali ambayo imesababisha kutokea kwa ngumi hizo," alisema.

Akizungumzia mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi, alisema anaufahamu na baada ya barabara kupita katika kanisa hilo, Jiji walitoa viwanja vya hisani ili waweze kuviuza na kuendelea na ujenzi wa kanisa mahali pengine walipopangiwa.

"Maelezo ya mchungaji ni kwamba viwanja vile viandikwe kwa majina binafsi inawezekana hapa ndipo walipokosea, ili viweze kuuzika na fedha ziendelee na ujenzi kama kuna mgogoro wameutengeneza wao sisi kama serikali tuliishamaliza kuwapa viwanja," alisema.

Hata hivyo, Katambi alionyesha kusikitishwa na kitendo cha waumini hao kupigana ndani ya ibada.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema jambo hilo bado wanaendelea kufuatilia.Nipashe ilipomtafuta mchungaji Malendaa kuzungumzia tuhuma hizo,  alisema kuwa viwanja hivyo vipo na wanatafuta wateja ili waviuze.

"Tatizo kuna baadhi ya waumini ni wakorofi wanaamini mimi nimeviuza bila kuwashirikisha," alisema. 

Habari Kubwa