Waziri aagiza ukaguzi maeneo yaliyovamiwa 

10Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
MWANZA
Nipashe
Waziri aagiza ukaguzi maeneo yaliyovamiwa 

HALMASHAURI zote nchini zimetakiwa kupitia upya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii kama vile makaburi, maeneo ya wazi, ujenzi wa taasisi za umma na masoko ili kujiridhisha kama bado yanafaa kwa matumizi yaliyokusudiwa au yamevamiwa. 

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, alitoa agizo hilo jana wakati akikagua utekelezaji kupitia maeneo yaliyovamiwa katika wilaya za Ilemela na Nyamagana.

Mabula alikemea kitendo kinachofanywa na baadhi ya halmashauri nchini kutolipa fidia katika maeneo zinayoyatwaa hali inayosababisha kuzalisha migogoro isiyo ya lazima na uvamizi mpya katika maeneo hayo.

“Halmashauri zote nchini naziagiza kupitia upya maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za kijamii ili tujue maeneo hayo yamevamiwa kwa kiasi gani, tuwafanyie urasimishaji wananchi walipe kodi ya serikali. Kama eneo bado halijavamiwa basi tulilinde ili lisiendelee kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa,” alisema. 

Pia aliwataka wataalamu wa ardhi nchini kuacha kukaa ofisini na badala yake waende kwa wananchi ili kuepuka kuitia hasara serikali kwa kutoa taarifa zisizo na uhakika.

Aliwatoa hofu wananchi wa mitaa ya Nyagungulu, Mwambani na Bukengwa yaliyoko kata ya Ilemela kuwa serikali itaendelea kutatua migogoro ya ardhi kwa kuzingatia haki, sheria na ubinadamu.

Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula, mbali na kumpongeza Naibu Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya, alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuunda timu ya mawaziri kupitia maeneo yote yenye changamoto za ardhi, huku akiiomba Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuhakikisha ulipaji fidia kwa wananchi wenye migogoro ya ardhi unafanyika.

Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa, Makwasa Biswalo, alisema  ukaguzi maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za kijamii ulianza Septemba 30, mwaka huu na kumalizika Oktoba 4 kabla ya kuongezwa siku nne.

Hata hivyo, kamishna huyo msaidizi aliomba ushirikiano kutoka kwa wananchi na viongozi ili kukamilisha ukaguzi huo haraka na kwa ufanisi.

Habari Kubwa