Dar ‘kidume’ kwa magonjwa ya akili

10Oct 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Dar ‘kidume’ kwa magonjwa ya akili

MIKOA mitano imetajwa kuwa na wagonjwa wengi wenye magonjwa ya akili, huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kuwa na idadi kubwa.

Hali ya kimazingira ukiwamo ugumu wa maisha na matumizi ya vilevi, vimetajwa ni miongoni mwa viashiria vinavyochangia tatizo hilo kwa maeneo ya mijini kuliko vijijini.

Akizungumza na Nipashe jana, Daktari wa Afya ya Akili katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Omary Ububuyu, alisema takwimu zilizopo kwa miaka mitatu kuanzia 2016 hadi 2018 zinaonyesha  magonjwa ya akili yameongezeka kutoka 301,000 hadi  356,000.

“Kwa mwaka 2016 kulikuwa na wagonjwa 301,000 inahusisha magonjwa ya akili, kifafa na matumizi ya kilevi,” alisema wakati akizungumzia  maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani leo.

Alieleza kuwa magonjwa ya kifafa kwa ujumla wake baadhi yametibiwa kwenye idara ya magonjwa ya akili na mengine nje ya idara ambapo yana takribani asilimia 50 ya wagonjwa wote.

“Sasa magonjwa haya matatu katika takwimu za Wizara ya Afya na Tamisemi zinaonyesha katika vituo vya afya takribani wagonjwa 356,000 kwa mwaka 2018, pia asilimia 50 ya magonjwa ni ya akili na nyingine ni kifafa,” alisema na kuongeza:

 “Hii ni kwa hospitali ya mkoa na vituo vya afya, hapa hatujahusisha takwimu kutoka hospitali kama Muhimbili na Mirembe na hospitali zingine kubwa.”

Mikoa vinara

Dk. Ububuyu alisema mijini kuna wagonjwa wengi zaidi ambapo takwimu hizo zinaonyesha Dar es Salaam inaongoza kuwa na wagonjwa asilimia 20 bila kujumuisha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Mkoa mwingine ni Kilimanjaro, Tanga, Morogoro na Mwanza,  yote mitano ipo juu na hali hii hapo katika magonjwa ya akili peke yake hata magonjwa yasiyo ya kuambukiza hali ipo hivyo hivyo.”

“Dar es Salaam inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza halafu mikoa mingine inafuata, Dar es Salaam ina asilimia 20, Kilimanjaro 9, na mingine asilimia 7 hadi 5. Mikoa yenye wagonjwa kidogo ni Katavi 0.1, Rukwa 4, Songwe pia ina asilimia chache ya wagonjwa,” alisema.

Hata hivyo, alisema hali za kimazingira na vilevi ndizo zinazochangia zaidi kuliko viashiria vya kibaiolojia kwenye maeneo ya mijini kuliko vijijini.

“Kuna vihatarishi vinavyosababisha magonjwa ya akili ambapo kikubwa namba moja ni vinasaba, vitu vya kibaiolojia kuna kupata majeraha ambayo yanaathiri ubongo, baadhi ya magonjwa yanayopanda kichwani ikiwamo malaria, HIV.”

“Pia matumizi ya vilevi kama pombe, bangi, sigara na vilevi vingine kwa kuwa vilevi kazi yake kubwa ni kushusha uwezo wa ubongo kufanya kazi na mambo yaliyokuwa yakitarajiwa,” alisema.

Mtaalamu huyo alisema: “Utakuta vilevi vingi vinaweza kuwa vihatarishi, unaweza ukatumia bangi ukaumwa, pia hali ya kijamii yaani ya kiuchumi ikiwamo ugumu wa maisha yaani kuwa na hali ngumu kupita kiasi ambayo mtu hawezi kuimudu kama kufiwa mtu akashindwa kustahimilivu maumivu ya kupoteza kitu anachokipenda kama kazi, mwenza, rafiki au ndugu.”

Alieleza  wakati mwingine pia kuwapo katika mazingira ya ukatili, ajali kubwa kwa mfano ajali  ya moto Morogoro kuna baadhi ya watu hawakuathirika na moto, lakini walishuhudia yale yaliyotokea kwa hiyo hao wanaweza kuathirika kiakili.

Kuhusu watoto wadogo,  alisema kwa watoto wadogo kinachochangia kwa kiasi kikubwa kushinda sehemu nyingine zote ni vitendo vya ukatili wa aina zote.

“Kadhalika, kuugua magonjwa mengine kama saratani au ugonjwa mwingine wowote mkubwa unaweza kuwa kihatarishi cha kupata magonjwa hayo.

“Lakini kuishi na mtu anayetumia vilevi kupindukia, au matatizo ya akili ambayo yamekosa kabisa huduma inaweza kusababisha mtu kuwa kwenye mazingira magumu ambayo yanaweza kumpeleka kwenye vihatarishi,” alisema.

Utafiti uliofanyika

Dk. Ububuyu alisema baadhi ya utafiti uliofanyika ukiwamo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambao ulifanyika kujua ukubwa wa tatizo na Tanzania ilijumuishwa, na kuonyesha takribani asilimia moja ya watu wana matatizo makubwa ya magonjwa ya akili kupita kiasi.

“Hii ni ile ya kuchanganyikiwa kupita kiasi, kwa hiyo kama kwetu tuna idadi ya watu milioni 50, hivyo watu takribani milioni 5 wana matatizo,” alisema.

“Kuna utafiti pia alifanya Prof. Joseph Mbatia, alifanyia Dar es Salaam na mikoa mingine ambapo inaonyesha takribani asilimia 8-15 ya Watanzania ambao wanaweza kuwa na matatizo ya akili kwa ujumla wake ikiwamo sonona,” alisema.

Hali ya utoaji huduma

Alibainisha  hali ya utoaji huduma inaimarika kwa kuwa kuna vituo vya afya na hospitali nyingi zimejengwa, huku changamoto ni kuwapo kwa idadi ndogo ya watumishi wanaotoa huduma za afya ya akili katika ngazi ya afya ya msingi.

“Katika mikoa yote 26 yenye hospitali za mikoa 28 kuna madaktari bingwa wawili ambao wamekuwa wakitoa huduma kwa miaka mitatu na wengine wengi wapo katika hospitali za rufani,” alisema.

Kadhalika, alisema wanategemea kupata uwezeshaji wataalamu  kutoka hospitali za taifa, lakini kutokana na idadi ndogo ya wataalamu hawawezi kuwatawanya waliopo kwa kuwa wao pia ni walimu na wanafanya mambo mengine.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirikisho la Afya ya Akili Duniani (WFMH) ya mwaka 2017, mtu mmoja kati ya wanne ana matatizo ya akili.

Habari Kubwa