Bila ushirikiano sasa Afrika inajiua yenyewe 

10Oct 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Bila ushirikiano sasa Afrika inajiua yenyewe 

BIASHARA miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), inatetereka na mambo si mazuri.

Ni masuala yanayoibuka kwenye mkutano wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), wakati wa kujadili ripoti ya Kamati ya Biashara na Uwekezaji ya EAC ya mwaka 2016.

Hapo inaelezwa kuwa thamani ya biashara miongoni mwa nchi wanachama kwa mwaka huo, ilishuka kutoka dola bilioni 3.2 mwaka 2015 hadi kufikia dola bilioni 2.6.

Moja ya sababu zinazotajwa kuchangia kushuka kwa biashara katikaripoti hiyo ni pamoja na kuendelea kuwapo kwa vikwazo visivyo vyakodi au ‘none tariff barriers’ (NTBs).

Aidha, kukosekana kwa mifumo inayodhibiti ufanyaji biashara na kingine ni mataifa wanachama kushindwa au kukataa kuridhia mikataba ya biashara baina yao bilasababu yoyote ya msingi.

Jambo hilo si jema kwa afya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayokusudia kuwa na ushirikiano ili kufikia mtangamano.

Lakini tatizo hilo si kwa EAC pekee huenda ni Afrika nzima.

Masuala yanayohusu ushirikiano yamekuwa magumu kufikiwa kutokana na wanachama kufikiria kibinafsi zaidi.

Wakati mambo yanashindikana kuanzia biashara na maingiliano ya raia wa EAC na hata kwenye Umoja wa Afrika (AU), ni wakati wa kujikumbusha kuwa ili usikike na ushawishi wako kukubalika na wengine ni lazima uwe na nguvu.

Nguvu hizo ni kiburi cha kiuchumi, umahiri wa teknolojia, uwezo wa kijeshi na mamlaka za kisiasa za kushawishi na kuyalazimisha mataifa mengine kukusikia na kukutii.

Ndiyo maana mataifa yenye msuli huo kama Marekani na China ambalo ni taifa la pili kwa uchumi mkubwa duniani yanathamini muungano, umoja na mtangamano.Si hivyo hata Umoja wa Ulaya (EU) unasimama imara na kulinda muungano wake licha ya kuwapo na sekeseke kama vile Uingereza kujitoa.

Umoja na ushirikiano ndiyo msingi mkubwa wa kuwa imara kiuchumi, kiteknolojia na hata kiushawishi.

Leo hii dunia inazitazama China, Marekani, India na EU kama madola yenye nguvu na ambayo yana ushawishi mkubwa mno (influence).

Amerika inaposimamia jambo leo ni lazima dunia itasikiliza, aidha China inapoinuka kila taifa linasikiliza kufahamu China inasema nini. 

Si hivyo tu hata India, Umoja wa Ulaya na pengine mataifa ya Amerika Kusini hasa Mexico.Afrika isijidanganye kuwa itakuwa inaendeleza ubinafsi wa kila nchi kujifanyia inavyotaka na kukataa mtangamano na ushirikiano.

Kama Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan hazitaweza kufanya biashara na kushirikiana zitawezaje kushirikiana na China, India na EU?

Kama inakuwa vigumu kuwa na umoja na ujirani ndani ya Afrika itawezekanaje kuwa na Dola la AU ambalo nalo linatakiwa kusimama kama China au India au EU kwenye kutetea mambo yake iwe kiuchumi au kisiasa?

Inabidi Afrika na pia EAC, kujikumbusha kila wakati kuwa umoja ndiyo silaha pekee ya ushindi.Kama Marekani ina majimbo 52, Afrika nayo yenye nchi 53 inashindwaje kuwa na mtangamano kama ilivyo Marekani?

Kwanini mataifa ya Afrika yasiungane  na kuwa na dola la AU ambalo ndilo litakalokuwa mwanzo wa mafanikio ya kila kitu ikiwa ni pamoja na kuondoa umaskini na uasi wa kisiasa? Afrika Mashariki inahitaji sana kuungana na kufanya biashara na miradi ya maendeleo pamoja kwa kuunganisha nguvu, kama ilivyo China na India.

Ni wazi kuwa hakuna mafanikio kama Waafrika hawatajiunga na kuamua kufanya mambo kwa ushirika.

Baadhi ya wabunge wa EALA wanasema nchi wanachama zimejawa nahofu ‘isiyofahamika’ ya kuogopa muungano au mtangamano.

Wanaona kuwa kuna woga uliojaa miongoni mwawanachama wa EAC yenye nchi sita wanachama, kuwa ndiounaochangia kuua jumuiya kwa kuwa unasababisha malengo ya waasisi wajumuiya kushindwa kufikiwa.

Ni lazima Afrika pamoja na EAC kutekeleza maamuzi wanayojiwekeawenyewe kwa ajili ya manufaa yao na  watu wao kwa sababu bila mtangamano hakuna maendeleo.

Ni kitu gani kinachosababisha wanachama kuogopana na kushindwa hata kuridhia masuala na mikataba waliyokubaliana wenyewe kwa miongo kadhaa?Bila kuwa na umoja mambo yataendelea kuwa mabaya kwa Afrika na watu wake watabaki kuwa maskini, wagonjwa, wajinga na walio nyuma kimaendeleo kwa kuwa tu, viongozi wamekataa ushirikiano.

Kwa mfano, kama Tanzania haiwezi kufanya biashara na Uganda, itafanyaje uwekezaji na ushirikiano na  mataifa mengine?

Ni lazima kujirekebisha na kuondoa   tofauti hizi kwa kuwa China na Afrika na mataifa mengine ya Mashariki ya Mbali kama Indonesia, Malaysia na Korea yalikuwa kwenye kiwango kimoja cha kiuchumi na Afrika miaka ya 1960, lakini hao umoja na ushirikiano umewavusha, Afrika na EAC zinangoja nini?

Ni wakati wa kutekeleza hayo ambayo viongozi wa Afrika wameyaona na yamethibitisha kuwa umoja ni ushindi na ndiyo mafanikio popote duniani.

Habari Kubwa