Bravo kuwapumzisha wazee wa mahakama

10Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Bravo kuwapumzisha wazee wa mahakama

MAHAKAMA ya Tanzania imesikia kilio cha muda mrefu, ambacho kimekuwa kikitolewa na baadhi ya watu wenye mashauri mahakamani dhidi ya wazee washauri wa mahakama.

Wazee hao wamekuwa wakilalamikiwa kuwa wanachangia kuchelewesha kumalizika kwa  mashauri mahakamani.

Ni kweli kwamba ulikuwa uamuzi mzuri wa kuwa na wazee washauri katika mahakama zetu kwa kuwa walikuwa wanasaidia kutoa ushauri kwa majaji na mahakimu kwa kutumia uzoefu wao, busara na pia kuijua vizuri jamii wanayoishi nayo.

Kwa kuzingatia hayo, kwa muda mrefu walikuwa wakiwasaidia majaji na mahakimu kupata maoni na ushauri kabla ya wakati wa kusikiliza kesi na kuandika hukumu.

Hata hivyo, kutokana na mapungufu mbalimbali ya washauri hao ambayo yalisababisha malalamiko dhidi yao, mahakama imefanya uamuzi wa kutokuwatumia, isipokuwa katika baadhi ya kesi.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Eliezer Feleshi, amesema Mahakama inakusudia kupunguza kuwatumia wazee hao katika kuamua mashauri mahakamani.

Badala yake amesema itabaki ikiwatumia katika mashauri ambayo yataonekana yana ulazima wa kuwatumia.

Akizungumza wilayani Bunda mkoani Mara katika ziara ya kikazi kukagua shughuli za Mahakama, Jaji Kiongozi alisema wazee hao watatumiwa na Mahakama kwenye mashauri ambayo yatakuwa na ulazima wa kuwatumia, lakini yale ambayo siyo lazima, wataacha kutumiwa.

Jaji Kiongozi alisema baadhi ya wazee washauri wa Mahakama hujihusisha na vitendo vya rushwa na wakati mwingine huwatisha mahakimu wanapokuwa wakitekeleza wajibu wao.

Alisema matumizi ya wazee washauri wa Mahakama wakati mwingine husababisha mashauri kuchelewa kumalizika kutokana na kuchelewa kwao kufika mahakamani na kusababisha mashauri kutokusikilizwa kwa wakati.

Sababu zilizotolewa na Jaji Kiongozi za kuacha kuwatumia wazee washauri ni za msingi kwa sababu bila kuchukuliwa uamuzi huo, kunaweza kuathiri shughuli za mahakama hasa kuchelewesha haki au kuwanyima haki watu wengine.

Inapofika mahali washauri hao wakajiingiza katika vitendo vya rushwa au kuwatisha mahakimu, ni dhahiri kwamba wanakuwa wamekosa sifa na uhalali wa kuishauri mahakama. Pia wadau wa mahakama na wenye kesi hawawezi kuwa na imani kwao tena.

Tunakubaliana na mahakama kwa kuchukua hatua hiyo kwa lengo la kurejesha imani ya umma kwa chombo hicho cha kutoa haki nchini.

Tunaona njia nzuri ya kuwawezesha majaji na mahakimu kupata ushauri mpana wakati wa kusikiliza mashauri, ni kufikiria uwezekano wa kuwatumia wataalamu hususan wa fani ya kesi husika.

Kwa mfano, kama kesi inahusu masuala ya ardhi, basi inaweza kuwatumia watu wenye utaalamu wa sekta hiyo, wakiwamo wastaafu. Hata hivyo jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa watu hao ni waadilifu, waaminifu na wenye weledi.

Tunashauri kuwa mahakama iendelee kuweka utaratibu mzuri wa kusikiliza malalamiko ya wananchi yanayoonekana kuathiri utoaji wa haki, na kuchukua uamuzi wa haraka baada ya kuyafanyia uchunguzi wa kina.

Tunaamini kuwa mahakama haitaishia kuwaondoa wazee washauri tu, bali watumishi wake wote ambao watabainika kujihusisha na vitendo vya ukosefu wa maadili.

Hilo likifanyika, mkakati wa chombo hicho wa kupunguza malalamiko ya rushwa dhidi yake litakuwa limefanikiwa.

Habari Kubwa