Mtuhumiwa wa wizi benki abambwa gesti na mil. 37/-

12Oct 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Mtuhumiwa wa wizi benki abambwa gesti na mil. 37/-

MTUNZA fedha wa benki ya Exim tawi la Dodoma, Martine Temu (33), anayedaiwa kuiba Sh. milioni 141.9, amedakwa na jeshi la polisi akiwa amejificha kwenye nyumba ya kulala wageni mkoani Singida.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma, SACP Gilles Muroto, akionyesha kwa waandishi wa habari jijini humo jana, fedha taslimu Sh. milioni 37, zilizokamatwa na jeshi hilo, zinazodaiwa kuibwa katika Benki ya Exim, tawi la Dodoma, Agosti 29 mwaka huu. Fedha hizo ni kati ya zaidi ya Sh. milioni 140 zilizoibiwa katika benki hiyo. PICHA: RENATHA MSUNGU

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema jana kuwa wizi huo ulitokea Agosti 29, mwaka huu na mtuhumiwa alitokomea kusikojulikana baada ya tukio hilo. 

"Aliiba fedha za Kitanzania milioni 120, USD 9,513 (Sh. milioni 21.8) na Euro 50 (Sh. 125,890). Baada  ya kufanya wizi alitoroka kwenda mafichoni. Msako mkali ulifanyika na kufanikiwa kumkamata mkoani Singida akiwa amejificha kwenye nyumba ya wageni iitwayo Manonga," alisema.

Muroto alisema mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa na Sh. milioni 37.5 kati ya fedha anazodaiwa kuiba. 

"Yupo mshiriki mwingine jina tunalihifadhi na msako mkali dhidi yake unaendelea. Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote,"alisema.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limemkamata Isack Okwango (27)  mkazi wa Buzuruga, Mwanza na Buguruni jijini Dar es Salaam katika nyumba ya kulala wageni ya Erickson Lodge iliyoko Makole  jijini hapa akiwa na jeki moja, bisibisi na simu tatu za wizi, kamera, komputa mpakato moja aina ya Toshiba na kisu.

Kamanda alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Oktoba 6, mwaka huu, akiwa katika nyumba hiyo na amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa tuhuma za kuvunja nyumba usiku na amekuwa akihama mikoa kwa ajili ya kufanya uhalifu.

Wakati huo huo, Mkazi wa Nyakato, Ashraf Sani (31) amekamatwa kwa tuhuma za wizi wa magari yaliyoegeshwa kwa muda katika sehemu za kumbi za starehe kwenye sherehe na mikutano.

Muroto alisema mtuhumiwa huyo alikuwa amepanga chumba katika nyumba ya kulala wageni Sweetland iliyoko Bahi Road jijini hapa.

Alisema mtuhumiwa huyo amekamatwa akiwa na rimu tisa, matairi matano, jeki mbili na spana.

Kamanda huyo alisema mbinu anazotumia ni kutumia gari lake lenye namba za usajili T 793 CFT Nissan kulisogeza karibu na gari analotaka kuiba na kuweka jeki na kufungua matairi.

Habari Kubwa