MCT yaboresha tuzo uandishi wa habari 

12Oct 2019
Elizaberth Zaya
Nipashe
MCT yaboresha tuzo uandishi wa habari 

BARAZA la Habari Tanzania (MCT), limezindua rasmi Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania mwaka 2019, huku likiondoa baadhi ya makundi na kuingiza mapya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya EJAT, Kajubi Mukajanga

MCT kupitia Kamati ya Maandalizi ya Tuzo za Umahiri, ilisema jana kuwa imeongeza makundi mapya matatu ya uandishi wa habari za ubunifu na maendeleo ya watu na uandishi wa habari za hedhi salama na afya ya uzazi.

Makundi yaliyoondolewa ni habari za usalama na ubora wa chakula, kodi na mapato, na habari za afya.Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,   Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya EJAT, Kajubi Mukajanga, alisema ikiwa ni mara ya 11 kufanyika kwa tuzo hizo, tayari zimezaa matunda.

'Lengo kubwa la kuanzisha mashindano haya lilikuwa kuhamasisha waandishi wa habari kufanya kazi kwa bidii na ufanisi zaidi, kuhakikisha wanafanya kazi zinazoleta matokeo chanya na kuacha alama. Tumeshuhudia hayo yanafanyika na ndiyo mafanikio tuliyokuwa tunayataka na ni furaha kubwa kwetu," alisema Mukajanga.

Katika awamu ya 11 ya mashindano hayo, alisema habari zitakazoshindaniwa ni kutoka makundi 20  zikiwamo tuzo ya uandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha; uandishi wa habari za michezo na utamaduni; uandishi wa habari za biashara na kilimo; uandishi wa habari za elimu; uandishi wa habari za utalii na uhifadhi na uandishi wa habari za uchunguzi.

Kajubi ambaye ni Katibu Mtendaji wa MCT, Makundi aliyataja makundi mengine kuwa ni uandishi wa habari za takwimu; uandishi habari za haki za binadamu na utawala bora; mpiga picha bora magazeti.

Mengine ni mchora katuni bora; uandishi wa habari za jinsia; uandishi wa habari za wazee; watoto; habari za gesi, mafuta na uchimbaji madini; habari za afya ya uzazi; habari za ubunifu na maendeleo ya watu; habari za usalama barabarani; hedhi salama na kundi la wazi.

Alisema kazi zinazotakiwa kuwasilishwa ni zile ambazo zimechapishwa kuanzia Januari hadi mwisho wa Desemba mwaka huu.

 Mukajanga alisema uwasilishwaji wa kazi hizo utafanyika kuanzia Oktoba 11, mwaka huu,  hadi Januari 31, mwakani.

Mtaalamu wa Mawasiliano kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Ubunifu (HDIF), Hannah Mwandoloma, ambao ni miongoni mwa wadhamini wa tuzo hizo katika kundi la tuzo za uandishi wa habari za ubunifu na maendeleo ya watu, alisema wameamua kudhamini tuzo hizo kutokana na umuhimu wake katika taifa.

Mwandoloma alisema ili nchi yoyote ipige hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi ni lazima kuwe na watu wanaofanya kazi za ubunifu.

Alisema lengo la kudhamini kundi hilo ni kuhamasisha waandishi wa habari kufichua kazi mbalimbali za kibunifu zinazofanywa katika maeneo mbalimbali ya nchi ili waweze kusikika na kusaidiwa kwa lengo la kuchangia maendeleo katika nchi.

Pia alisema uandishi wa habari za ubunifu zitawasaidia wabunifu wenyewe kutambua sera zilizopo nchini katika kufikia malengo yao.

Naye, Mwenyekiti wa Mtandao wa Wadau wa Hedhi Salama, Wilhelmina Malima, alisema wamemua kushiriki katika tuzo hizo ili kuhamasisha waandishi wa habari kuandika habari ambazo zitasaidia kuvunja ukimya uliopo katika jamii na kuongeza upatikanaji wa taarifa na kujenga miundombinu wezeshi kwa watoto wa kike.