Jafo awachongea Ma-RC kwa Rais 

12Oct 2019
Beatrice Moses
Nipashe
Jafo awachongea Ma-RC kwa Rais 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, amemwomba Rais John Magufuli, kupokea dokezo lake la mapendekezo ya kuwachukulia hatua viongozi wa mikoa na wilaya ambao watafanya vibaya kwenye uandikishaji wapigakura uchaguzi wa serikali za mitaa.

Pia amesema uandikishaji wa wapigakura kwa ajili ya uchaguzi huo si wa kuridhisha kwa mikoa yote nchini na kwamba kinachokosekana ni uhamasishaji.

Jafo aliyasema hayo jana mbele ya Rais wakati wa mkutano wa hadhara baada ufunguzi wa barabara ya Mpanda – Uvinza mkoani Katavi, ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kiongozi huyo.

Kwa mujibu wa Jaffo, mikoa iliyofanya vizuri kuwa ni pamoja na Iringa ambao imefikisha asilimia 53 ukifuatiwa na Mbeya, Songwe na Tanga.

Alisema katika tathmini hiyo, Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia nane huku Kilimanjaro ikiwa na asilimia 12 na Arusha asilimia 13.

"Naomba uridhie uandikishaji unaisha Ocktoba 14, mwaka huu. Haiwezekani  siku ya mpira wa Simba na Yanga watu wote wanaenda uwanjani lakini siku ya uandikishaji watu wanasuasu. Endapo siku saba zitakwisha na kuna mikoa haijafika hata asilimia 50 nitaomba nilete dokezo kwako," alisema.

"Kuna wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa na wilaya, kuna wakurugenzi itakapobainika watu walizembea katika kuhamasisha watu kujiandikisha, nitaomba wachukuliwe hatua," alisema. 

Alisema agenda ya uchaguzi wa serikali za mitaa ndiyo inayotoa mchakato wa maendeleo na kwamba ikibainika kuwa watu wengi walizembea kuhamasisha watu kujiandikisha, atapeleka pendekezo maalum kwa Rais Magufuli  kwa hatua zaidi.