Watalii kutoka Israel wamiminika Moshi, Arusha

14Oct 2019
Godfrey Mushi
HAI
Nipashe
Watalii kutoka Israel wamiminika Moshi, Arusha

MIJI ya kitalii ya Moshi na Arusha, imeanza kufurika idadi kubwa ya makundi ya watalii kutoka nchini Israel, baada ya serikali kupokea wageni hao zaidi ya 720 waliotua nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii (TTB), Devotha Mdachi

Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii (TTB), Devotha Mdachi, akizungumza juzi usiku, wakati wa kuwapokea watalii hao alisema ujio wa wageni hao ni juhudi kubwa za utangazaji wa vivutio vilivyopo nchini uliofanywa na bodi hiyo kwa kushirikiana na balozi zake.

"Watalii hawa ni matokeo ya juhudi za utangazaji ambazo zimefanywa na Bodi ya Utalii Tanzania, lakini kwa kushirikiana na wadau kutoka sekta binafsi na ubalozi wa Tanzania nchini Israel. Hii ni ishara kwamba sasa soko la Israel limefunguka na tunategemea kwamba idadi ya watalii kutoka nchi ya Israel itaongezeka mara dufu," alisema.

Ndege nne zenye watalii kutoka nchini humo ziliwasili katika Uwanja wa Ndege Kimataifa wa KIA uliopo Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro juzi usiku, zikiwa na maelfu ya watalii.

Kwa mujibu wa TTB, watalii hao watapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali zikiwamo hifadhi za taifa ili kujionea utajiri huo wa maliasili na baadaye waweze kwenda kushawishi watalii wengine katika nchi zao kuja kujionea wenyewe ni kwa jinsi gani Tanzania isivyosahaulika.

Kwa upande wake, Jaji mstaafu Thomas Mihayo, akizungumza baada ya ndege zilizowabeba watalii hao kuwasili alisema: "Niwaombe wote ambao wanahusika na mambo ya utalii wachukue maanani ya kwamba watalii ni lulu, kikubwa zaidi wawathamini. Na ndugu zangu sasa katika tasnia ya utalii wajifunze zaidi."

Idadi hiyo ya watalii kutoka nchi ya Israel imeongezeka nchini, hatua inayoifanya kutoka nchi ya 20 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hadi kuwa nchi ya sita kwa kiwango cha watalii wanaotembelea vivutio vya utalii ndani ya nchi.