Watanzania waaswa matumizi ya dawa

14Oct 2019
Ibrahim Joseph
DODOMA
Nipashe
Watanzania waaswa matumizi ya dawa

WANANCHI wameshauriwa kuacha tabia ya kutumia dawa bila ushauri na wataalamu wa afya ili kujiepusha na madhara yatokanayo na matumizi holela ya dawa.

Hayo yalielezwa na kiongozi wa timu ya madaktari bingwa, Dk. Nassoro Mzee, alipokuwa na waandishi wa habari kwenye matibabu ya kibingwa yaliyotolewa katika Viwanja vya Msikiti wa Nughe, jijini hapa.Dk. Mzee alisema matumizi holela ya dawa hizo yanasababisha kujenga usugu wa magonjwa.

"Hizi dawa zinaponya, lakini pia ni sumu matumizi yake yanatakiwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya hivyo matumizi holela  yanaweza kusababisha madhara au kifo hivyo wanatakiwa kuchukua tahadhari hiyo," alisema.

Alisema wananchi wanatakiwa kumwona  mtaalamu wa afya ili kuchukuliwa vipimo na kujua aina ya ugonjwa unaomsumbua na ndipo wataweza kuandikiwa aina ya dawa za kutumia.

"Kwa kawaida ugonjwa wowote unapoingia kwenye mwili wa mtu lazima utasikia homa, lakini aina ya ugonjwa itaonekana kwa njia ya vipimo hivyo tusitumie dawa kabla ya kufika hospitali kumwona daktari akupe ushauri," alisema.

Kuhusu huduma hiyo, Mtaalamu huyo alibainisha kuwa timu hiyo ilikuwa ikitoa huduma matibabu ya kibingwa bure kwa wananchi, lakini dawa zilinunuliwa na uongozi wa msikiti huo na kutoa bure kwa wagonjwa.

Aliongeza kuwa katika kambi hiyo walibaini magonjwa mengi yanayowasumbua wagonjwa  waliofika kwao kuwa ni shinikizo la damu, uzito uliopitiliza na kinamama wengi kusumbuliwa na tatizo la hedhi.Mmoja wa wagonjwa, Suleman Mruta aliomba matibabu hayo kuwa endelevu na kushukuru timu ya madaktari hao kuona umuhimu wa kutoa matibabu bure wananchi.

"Kama mnavyojua gharama ya matibabu ni kubwa leo hii tumeweza kukutana na madaktari hawa jambo ambalo ukienda Hospitali ya Mkoa au Benjamini Mkapa kuwaona ni gharama, lakini leo tumehudumiwa bure," alisema.

Kwa upande wake, Imamu wa Msikiti wa Sunni Nughe, Shekhe Abdalah Juma, alisema kilichowasukuma kuomba kutoa huduma za afya hapo ni kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa na wakati mwingine baadhi ya watu hushindwa kumudu.

Shekhe Juma alisema katika siku hiyo wananchi walichangia lita zaidi ya 100 za damu na watu  zaidi ya 200 walifika katika kambi hiyo kupata  huduma za kiafya.Alisema matibabu hayo yalishirikisha wananchi wote bila kujali itikadi ya dini na yatakuwa endelevu kutokana na mwitikio wa watu wengi.

Habari Kubwa