Mbia wa Kambarage, kuanzia Butiama hadi Ikulu

14Oct 2019
Mashaka Mgeta
Butiama
Nipashe
Mbia wa Kambarage, kuanzia Butiama hadi Ikulu
  • · Amsifu JPM kurejesha nyayo

INGAWA si rahisi kumfananisha moja kwa moja na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, lakini zipo ishara na matendo ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli za ‘kufuata nyayo’ za mwasisi huyo wa uhuru wa Tanganyika na baadaye Tanzania.

Mwalimu Julius Nyerere, enzi za ujana wake.

Ndivyo anavyoamini Wisigana Nyerere (86), kaka pekee aliyebaki katika uzao wa Mtemi Nyerere Burito ambaye ni baba mzazi wa Mwalimu Nyerere.

Wisigana aliyezaliwa mwaka 1933 ni mtoto wa tisa kuzaliwa kutoka kwenye tumbo la Mugara Mutiro, mke wa nane kati ya wake 22 wa Mtemi Nyerere Burito.

Ingawa historia ya maisha yake na Mwalimu Nyerere inatokea mbali, lakini Wisigana anasema ndiye aliyeongozana na Mwalimu Nyerere kutoka kijijini Butiama kwenda Pugu, alikokwenda kufundisha.

“Mwalimu Nyerere kwa vile alikuwa msomi na mimi niliishia darasa la tatu, alinichukua twende wote ili nikamsaidie kazi ndogo ndogo za nyumbani,” anasema Wigisana anayejishughulisha na shughuli za kilimo na ufugaji kijijini Butiama.

Makazi yake yamepakana na mji wa awali wa Mwalimu Nyerere alioujenga wakati akishiriki shughuli za kutafuta uhuru, kabla ya kurejea kwenye makazi ya baba yake, Mtemi Nyerere Burito yanayojulikana kwa Kizanaki kama Mwitongo, maana yake ni mahame.

KUJIUNGA TANU

Wisigana anasema, baada ya kuwasili Pugu mwaka 1953, Mwalimu Nyerere alishiriki shughuli za kisiasa zilizolenga kudai uhuru, hivyo kujikuta akikabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa wakoloni na baadhi ya Watanganyika (sasa Watanzania) walioanzisha upinzani dhidi yake.

Anasema haikuwa rahisi kumshauri Mwalimu Nyerere kuiepuka hatari iliyomkabili kwa kumtaka asiendelee na harakati za kudai uhuru, badala yake, yeye na wenzake waliendelea kumsaidia na kumtia moyo.

Wisigana anasema, mwaka 1954, TAA ilibadilika kuwa Tanganyika African Nation Union (TANU) na Mwalimu Nyerere aliendelea kuwa kiongozi wake.

Anasema ilipofika mwaka 1961, Tanganyika ilipata uhuru, yeye na dada zake wawili, Nyabhisenye na Nyakwe walikwenda kuishi Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam wakiwa na Mwalimu Nyerere aliyekuwa Waziri Mkuu na baadaye Rais wa Tanganyika (sasa Tanzania).

Wisigana anasema, baada ya kufika jijini humo, alipewa kazi ya kuwa mwangalizi wa mashamba ya serikali yaliyokuwa Mjimwema jijini Dar es Salaam na Iringa.

Anasema mwaka 1962, alirejea nyumbani kwake kijijini Butiama na kujishughulisha na kilimo na ufugaji, kazi zilizomfanya kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wa wakati huo.

Wisigana anasimulia licha ya maisha aliyoishi Ikulu, kurejea kwake kijijini hakukumsononesha kwa vile msingi wa maisha yake ulikuwa huko na kwamba hata Mwalimu Nyerere alikuwa anathamini maisha ya kijijini, licha ya kuwa kiongozi wa nchi.

Anasema kazi ya kwanza aliyoifanya ni kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la ukoo wa Mtemi Nyerere, lililogawanywa kwa wana-ukoo akiwamo yeye (Wisigana).

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, nyumba hiyo ya Mwalimu Nyerere ndiyo aliyoilenga wakati akihoji kujengewa nyumba kubwa kama atakayeishi humo ni tembo.

Maneno hayo aliyotamka wakati wa uzinduzi wa makazi yake aliyojengewa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) eneo la Mwitongo, mahali yalipokuwa makazi ya baba yake, Mtemi Nyerere.

Wisigina ambaye kwa sasa ameteguka mguu, anaishi kwenye eneo hilo akiwa hana usaidizi kutoka kwa watu na taasisi zilizokuwa karibu na Mwalimu Nyerere.

MWALIMU ALIUKABILI UPINZANI

Wisigana anasema, moja ya mambo yaliyomweka Mwalimu Nyerere katika hatari na tishio la kukata tamaa ni vikwazo kutoka kwa wakoloni na upinzani kutoka kwa Watanganyika wazawa, akiwamo (jina tunalo) aliyewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa TANU.

Anasema, ulikuwa wakati mgumu kwa vile, licha ya kuwapo vikwazo hivyo, haikuwezekana kumshawishi Mwalimu Nyerere aachane na harakati za kudai uhuru, badala yake wasaidizi wake akiwamo yeye (Wisigana) waliendelea kufuata maagizo yake.

Hata hivyo, anasema licha ya ushindani huo, Mwalimu Nyerere alijenga hoja kukabiliana na upinzani dhidi yake hadi kufanikisha kupatikana kwa uhuru.

HULKA YAKE KIJIJINI

Wisigana anasema wakati wa uhai, Mwalimu Nyerere alitenga muda wa kuishi na watu wa jamii yake katika kijiji cha Butiama, akiwa katika hulka na tabia zisizokuwa tofauti na anapokuwa katika majukumu yake ya kitaifa na kimataifa.

Anasema, yapo mambo mengi yaliyomchukiza hasa hongo zilizotawala kuanzia ngazi za chini kwenye jamii hadi kitaifa.

“Haya mambo ya hongo hongo yalimchukiza sana Mwalimu Nyerere, aliyachukia na hakutaka kabisa kusikia habari za hongo,” anasema.

Pia Wisigana anasema hali ya kupenda ubinafsi na kujilimbikizia mali inayopaswa kutumika kwa maslahi ya watu wengi, ilikuwa miongoni mwa machukizo kwa Mwalimu Nyerere.

“Kwa mfano, kama kulikuwa na mradi wa maji kwa ajili ya watu wa Bumangi (moja ya vijiji vilivyopo ukanda wa Zanaki), kisha akatokea mtu ama watu wanajiunganishia na kufanya yashindwe kuwafikia watu wengi, basi alikasirika sana,” anasema Wisigana.

Anasema, ufuatiliaji na hatua zinazochukuliwa na utawala wa Rais Dk. Magufuli hasa katika kudhibiti rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na kudhibiti wizi dhidi ya mali za umma, vinaashiria ‘kufuata nyayo’ za Mwalimu Nyerere.

“Kwa hali ilivyo sasa tunaiona serikali inatumia mbinu za Mwalimu Nyerere na hali ikiendelea hivi, mambo mengi aliyokuwa akiyasimamia (Mwalimu Nyerere) yatarejea hata kama si kwa kiwango kile cha awamu ya kwanza,” anasema.

KUPENDA VIKAO

Wisigana anasema jitihada zozote zinazofanywa kumuenzi Mwalimu Nyerere, zinapaswa kutoa kipaumbele kufanyika kwa vikao, ili kupata mawazo mapana zaidi yanayosaidia kufikia uamuzi sahihi kama alivyofanya (Mwalimu Nyerere).

“Viongozi wetu waendeleze utamaduni wa kukaa vikao, Mwalimu Nyerere alipenda sana vikao kuanzia kwenye ukoo wetu. Hata uamuzi aliokuwa anauchukua kwa sehemu kubwa ulitokana na majadiliano ya kwenye vikao,” anasema.

MAISHA YA KIDINI

Wisigina anasema Mwalimu Nyerere alipenda dini hasa Kanisa Katoliki, hadi alipobatizwa kwenye misheni (hivi sasa ni parokia) ya Nyegina mkoani Mara mwaka 1953.

Anasema, mbali na Nyegena, misheni Katoliki nyingine zilizokuwapo kwenye ukanda huo ni Bumangi na Busegwe.

“Baada ya kuingia kwenye ukatoliki na kubatizwa jina la Julius, Mwalimu Nyerere alianza kufundisha dini kwa Wazanaki, ingawa hakueleweka kwa urahisi,” anasema.

Anasema baada ya jitihada zake hizo, Mwalimu Nyerere aliamua kumleta Padri mmoja (ambaye hamkumbuki jina) kwenye misheni ya Magorombe iliyopo kijijini Butuguri na baadaye, akamwezesha ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Butiama alipokuwa akisali.

Anasema, wakati Mwalimu Nyerere akijiwajibika katika kueneza dini kupitia kanisa Katoliki, Mtemi Edward Wanzagi alijiunga katika kanisa la Last Church of God. Wakati huo walikuwa wakisali chini ya mti.

Wisigana anasema, licha ya kuwa kwake karibu na Mwalimu Nyerere, yeye mwenyewe hakubatizwa, kwa vile baada ya kushiriki mafunzo na kufikia ukomo wa kubatizwa, Mwalimu Nyerere aliondoka Pugu kutokana na mgongano wa kisiasa uliokuwapo.

“Nilishiriki mafundisho pale Pugu, lakini wakati nikikaribia kubatizwa, Mwalimu Nyerere, aliondoka na mimi nikaondoka, hivyo sikubatizwa hadi sasa,” anasema.

TAA NA TANU

Wisigana anasema baada ya chama cha Tanganyika African Association (TAA) kubadilika kuwa Tanganyika African Nation Union (TANU), alikabidhiwa kadi namba 14, hivyo kuwa miongoni mwa walioshiriki kuandikisha wanachama wapya.

Anasema, uandikishaji huo ulikabiliwa na vitisho kutoka kwa wakoloni, hivyo kuwalazimu kujificha na wakati mwingine kuwaandikisha wanachama wapya kwa usiri mkubwa.

SHANGWE ZA UHURU

Wisigana anasema Desemba 9, 1961 akiwa kijijini Butiama, dunia ilitangaziwa uhuru wa Tanganyika, hivyo kusababisha shangwe kubwa maeneo mengi ya nchi, lakini zaidi kijijini Butiama.

“Tulikesha tukipiga na kucheza ngoma, tulikula na kunywa vyakula vya kitamaduni, tukafurahi sana kwamba kijana wetu ametimiza utabiri wa baba yake,” anasema.

Kwa mujibu wa Wisigana, Mwalimu Nyerere alipaswa kuwa miongoni mwa Watemi, lakini baba yake, Mtemi Nyerere alikataa kwa sababu ya kuamini kwamba atakuwa na majukumu makubwa ya kitaifa.

“Mtemi Nyerere alisema Kambarage (Mwalimu Nyerere) hapaswi kuwa Mtemi kwa sababu utawala wake ni wa eneo dogo, lakini uwezo alionao utamfanya kuwa na majukumu kwa nchi nzima,” anasema.