Yanga puuzeni kelele  za chura mkijiandaa Caf

14Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Yanga puuzeni kelele  za chura mkijiandaa Caf

HATIMAYE wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Klabu ya Yanga imeanza maandalizi ya mechi yao ya mchujo kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kumfahamu mpinzani wao. 

Yanga imeangukia Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Zesco ya Zambia kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Na tayari Shirikisho la Soka Afrika (Caf), lenye dhamana na michuano hiyo, limeshaendesha droo ya michuano hiyo ambapo Yanga itakutana na Pyramids ya Misri ikianzia nyumbani katika Uwanja wa CCM Kirumba Oktoba 27, mwaka huu kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye.

Na endapo Yanga itapata matokeo ya jumla katika mechi hizo mbili nyumbani na ugenini, itafuzu moja kwa moja hatua ya makundi. 

Hata hivyo, baada ya droo hiyo kupangwa kumekuwapo na maneno mengi kutoka kwa wachambuzi wa soka wengi wakiamini, huo ndio mwisho wa safari ya Yanga kimataifa kwa msimu huu. 

Vitisho, au kujiaminisha kwa wanaovitoa kwa Yanga ni kutokana na uimara wa kikosi cha Pyramids ambacho kinaundwa na wachezaji kutoka Brazil na Colombia. 

Na si suala tu la kwamba wanatoka nchi hizo zilizopiga hatua kubwa kisoka, bali pia wanaamini wachezaji hao sita ambao gharama ya kuwanunua ni zaidi ya Sh. bilioni 80 za Tanzania, inamaanisha ni wa daraja la juu ukilinganisha na nyota wanaounda kikosi cha Yanga.

Pia kitendo cha Pyramids hadi sasa kushika nafasi ya pili nyuma ya vinara, Al Ahly kwenye msimamo wa Ligi Kuu Misri kunawafanya wengi waamini Yanga haitaweza kupenya hatua ya makundi.

Lakini pamoja na hayo yote, Nipashe tunaamini mpira hauchezwi kwa kuangalia gharama ya wachezaji husika kikosini wala nchi wanapotoka au nafasi yao kwenye ligi ya nyumbani. 

Ni kweli tunakubaliana na gharama ya mchezaji mara nyingi inatokana na ubora wake, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kujiaminisha kwamba inaweza kuibeba Pyramids mbele ya Yanga. 

Tulishuhudia msimu uliopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kelele kama hizo za wachambuzi na mashabiki wakiitoa Simba dhidi ya Al Ahly kabla na baada ya kuchezea kichapo cha mabao 5-0 nchini Misri. 

Wengi walijiamisha kuwa Simba ingechezea tena kichapo nyumbani na imani hiyo ikiongezeka kutokana na Al Ahly kuwa wachezaji ghali huku ikielezwa kuna mmoja aliyenunuliwa kwa zaidi ya Sh. bilioni tano za Tanzania ukilingabisha na kikosi cha 'Wekundu wa Msimbazi' hao ambacho kikosi kizima kilikuwa cha Sh. bilioni moja tu. 

Hata hivyo, Simba iliyokuwa ikitamba kwa kaulimbiu yao ya "Kila Mtu na Ashinde Nyumbani Kwao" ilifanya kweli na kuwachapa wanafainali hao wa Ligi ya Mabingwa Afrika wa msimu wa 2017/18.

Hivyo, hakuna kinachoshindikana kwa Yanga kufanya maajabu kama hayo ya Simba ama zaidi kama maandalizi ya kina, mipango na mikakati itafanyika kuelekea mechi hiyo huku ikipuuza kelele za wanaowabeza. 

Yanga imekamilika idara zote kasoro tu safu ya ushambuliaji ndiyo inayohitaji kusukwa vema ili iweze kutumia vema nafasi inazopata, lakini timu hiyo ikipaswa kupata mechi nyingi za kirafiki ama kuzitumia hizi za Ligi Kuu ili kuwa na muunganiko mzuri.

Hilo likifanyika, hakika itazima kelele zote hizi ambazo Nipashe tunaziona ni sawa na kelele za chura ambazo siku zote haziwezi kumzuia tembo kunywa maji. 

Habari Kubwa