Heko Bodi ya Ligi, viwanja  vibovu vinaumiza wachezaji

14Oct 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Heko Bodi ya Ligi, viwanja  vibovu vinaumiza wachezaji

WIKI iliyopita Bodi ya Ligi imevizuia viwanja vinne vya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza kutokana na ubovu kwenye sehemu ya kuchezea.

Ofisa Mtendaji wa Bodi hiyo, Boniface Wambura, amevitaja viwanja hivyo kuwa ni Uwanja wa Kinesi uliopo Magomeni jijini Dar es Salaam na Bandari uliopo Temeke.

Viwanja hivi hutumika kwa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara. Kwa upande wa Ligi Kuu, viwanja vilivyozuiwa ni Jamhuri Morogoro na Namfua uliopo Singida.

Wambura amesema wamevizuia viwanja hivi kutokana na ubovu kwenye eneo la kuchezea 'pitch' na kuagiza wahusika wawe wamerekebisha hali hiyo kabla ya mapumziko ya wiki ya mechi za kimataifa, yaani Kalenda ya Fifa kumalizika.

Akaongeza kuwa kama hali haitotengemaa basi wahusika watatakiwa watafute viwanja vingine mbadala hadi viwanja hivyo vitakaporekebishwa.

Ikumbwe kuwa Uwanja wa Jamhuri Morogoro unatumiwa na Mtibwa Sugar kama uwanja wake wa nyumbani, huku Singida United ikitumia Uwanja wa Namfua.

Hapa naona inaweza kuwa rahisi zaidi kwa Singida United, kwani inaweza kupeleka mechi zake kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, lakini tatizo linaweza kuwa ni kwa Mtibwa Sugar.Timu hiyo inatumia uwanja huo mkubwa, baada ya uwanja wake wa Manungu kuondolewa kwenye orodha ya viwanja vinavyotumika Ligi Kuu msimu huu kutokana na kutokidhi viwango.

Niipongeze Bodi ya Ligi kwani uamuzi huu unaweza kufanya viwanja hivyo vikarekebishwa. Kwa muda mrefu wamiliki wa viwanja hivi wametakiwa kurekebishe viwanja hivi, lakini baadhi yao wameonekana kama vile kuziba pamba masikioni, hivyo kama vikizuiwa inaweza kabisa kuwafanya wakaharakisha marekebisho.

Hata Rais John Magufuli, Mei 19, mwaka jana, wakati akiwakabidhi Simba Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Taifa, aliwataka wahusika na wasimamizi wa viwanja vingi nchini ambavyo vinamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuviboresha ili mpira uchezeke vizuri.

Kwa bahati nzuri kuna baadhi ya viwanja vinavyomilikiwa na CCM, vimeanza kukarabatiwa na kuwa vizuri na vyenye kuchezeka wakitii agizo hilo, mfano CCM Kirumba Mwanza na Samora Iringa, lakini baadhi kama vile Jamhuri na vingine ambayo havikutajwa bado havijafanyiwa matengenezo.

Viwanja vingi mikoani, pamoja na matatizo mengine, lakini ubovu mkubwa ni eneo la kuchezea ambapo wachezaji wamekuwa wakipata shida kuonyesha vipaji vyao, lakini kucheza kwenye mfumo ambao wamefundishwa na walimu wao.

Kutokana na hali hiyo ili kuendana na uwanja jinsi ulivyo, wachezaji wamekuwa wakibutua tu mipira kwa mtindo wa 'bora liende' na kusababisha hata mashabiki waikose burudani waliotaka kuiona baada ya kuingia uwanjani na pesa zao.

Nakumbuka kwenye mechi kati ya Mtibwa dhidi ya Mbeya City Septemba 29 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, wenyeji Mtibwa walifungwa bao ambalo halikutokana na ubora wa Mbeya City au mchezaji, bali ubovu wa uwanja, kwani lilipigwa shuti dhaifu ambalo kipa Shaaban Kado alitarajia kulidaka, mpira ulidunda sehemu kwenye uwanja huo mkavu na usio na majani, ukapoteza uelekeo kabla ya kuingia wavuni.

Waliokuwa wanaangalia mechi hiyo kwenye televisheni walishangaa sana, na huenda ikawa hili limesababisha zaidi kuisukuma Bodi ya Ligi kuzuia viwanja vya aina hiyo.

Viwanja hivyo pia vinasababisha wachezaji wengi kuwa majeruhi mara kwa mara, hivyo kwa hili Bodi ya Ligi wanastahili sifa na ifike mahali sasa ligi ichezwe kwenye viwanja ambavyo wachezaji watafurahia kucheza, wanaoingia kwa viingilio watafurahia kuangalia kandanda safi la ufundi, lakini hata wanaoangalia kwenye televisheni nao kufurahia wanachokiona.

Habari Kubwa