Muda wa kujiandikisha waongezwa

14Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muda wa kujiandikisha waongezwa

WAKATI leo ilikuwa ndiyo siku ya mwisho ya uandikishaji wa wapigakura kwenye daftari la orodha ya wapigakura, serikali imeongeza siku tatu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, kazi ya uandikishaji wapigakura kwenye daftari la orodha ya wapigakura itamalizika Alhamisi, Oktoba 17, mwaka huu.

“Waziri Jafo atangaza kuongeza siku tatu za uandikishaji wa wapigakura kwenye daftari la orodha ya wapiga kura. Sasa zoezi hilo litakamilika Oktoba 17, mwaka huu,” ilieleza taarifa hiyo.

MILIONI 11 WAJIANDIKISHA

Jafo alisema zoezi la uandikishaji limeendelea kupata mafanikio makubwa kwani hadi juzi zaidi ya watu watu milioni 11 waliweza kujiandikisha.

Jafo alisema wakati wa uandikishaji kulijitokeza changamoto mbalimbali kama vile kunyesha kwa mvua hali iliyosababisha watu kushindwa kujitokeza.

“Kutokana na changamoto hiyo, kutokana na misingi ya utoaji wa haki na kwa kuzingatia masharti ya kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa, natoa mwongozo kuwa zoezi la uandikishaji linaongezwa siku tatu zaidi,” alisema Jafo.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda jana alitoa taarifa ikieleza kuwa kuanzia leo atatembelea katika baa na sehemu za starehe kufanya ukaguzi wa kuwabaini watu ambao hawajajiandikisha.

“Ndugu zangu wenye klabu, baa na sehemu zote za starehe naomba wahamasisheni watu wenu kwenye maeneo yenu kuhakikisha wamejiandikisha na kesho (leo) miongoni mwa maeneo nitakayoyatembelea ni pamoja na baa… ni matumaini yangu nikifika nitakukuta ukiwa tayari umejiandikisha,” alisema Makonda.

Kazi ya uandikishaji wa wapigakura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu ilianza wiki iliyopita katika mikoa yote, lakini lilionekana kusuasua baada ya kuwapo kwa mwitikio mdogo wa wananchi kujitokeza.

Mkoani Dodoma, Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Binilith Mahenge, baada ya kujiandikisha kwenye kituo cha Nyerere, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa matokeo ya uandikishaji katika Wilaya ya Kondoa ni 37,762.

Alieleza kuwa tangu kuanza kwa kazi ya uandikishaji ni wastani wa watu 2,000 tu kwa siku.Kadhalika, katika Jiji la Dar es Salaam, hususani katika maeneo ya Magomeni, Kimara, Ilala, Kiondoni wananchi walionekana kusuasua kujitokeza katika uandikishaji.

Mkoani Morogoro, hadi kufikia Oktoba 10, idadi ya watu waliojitokeza kujiandikisha ilikuwa ni 203,553 kati ya watu waliotarajiwa kuandikishwa1,423,111.

Mikoa ya Dar es Salaam na Arusha ni miongoni mwa mikoa ambayo imeelezwa kuwa mwitikio wa wananchi kujiandikisha umekuwa wa kusuasua.