Tanzania yapewa angalizo ulaji ovyo

14Oct 2019
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
Tanzania yapewa angalizo ulaji ovyo

SHIRIKA la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), limetahadharisha Tanzania kuwapo ongezeko la idadi ya watu walio katika hatari ya kupata magonjwa sugu kutokana na mchanganyiko wa milo mibovu na maisha ya kutofanya mazoezi.

Mkurugenzi Mkazi wa FAO nchini, Fred Kafeero

Magonjwa yaliyotajwa ni shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo, kiharusi na aina fulani  ya saratani kutokana na mchanganyiko wa milo mibovu na aina ya maisha ya kutofanyisha miili kazi na uzito uliopindukia pamoja na unene uliopitiliza.

Tahadhari hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkazi wa FAO nchini, Fred Kafeero, wakati akiwasilisha hotuba yake katika ufunguzi wa mdahalo wa Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka 2019 uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mjini Morogoro.

Alisema walaji hususani  wa mijini hawana muda wa kutosha kuandaa vyakula nyumbani, hivyo wamejikuta wakiingia katika maisha ya kisasa ambayo kwa kiasi kikubwa yanategemea ununuzi wa bidhaa katika maduka makubwa, sehemu za kuandaa vyakula kwa haraka barabarani na kwenye migahawa ambayo milo hiyo ina wanga mwingi, sukari, mafuta na chumvi ambavyo sio rafiki kwa afya.

Alisema kutokana na hali hiyo, wataalamu wa afya wametangaza kwa sauti ya juu kwamba milo mibovu ni sababu kuu ya vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukizwa yakijumuishwa magonjwa ya moyo, kisukari na aina fulani za saratani.

Akizungumzua kuhusu lishe duni, alisema kama ilivyo katika nchi kadhaa, Tanzania nayo ina tatizo la watu kuwa na lishe duni inayosababishwa na milo ya watu kupungukiwa na viini lishe muhimu ambavyo vinahitajika na mwili kwa ajili ya afya njema.

Kafeero alisema hali hiyo ya lishe duni imekuwa ikisababishwa na ugonjwa, malezi na lishe mbovu ya utotoni, uchafu wa mazingira pamoja na kutofikia huduma mbalimbali za kijamii ikiwamo majisafi.

Hata hivyo alisema moja ya majukumu ya FAO ni kutomeza utapiamlo katika hali zote na pia ndio muhimili wa lengo la maendeleo endelevu namba mbili ya dunia bila njaa, na kwamba itahakikisha inasaidiana na Serikali ya Tanzania kusaidia usalama wa chakula na lishe.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alisema bado kuna tatizo la uzito na unene uliopitiliza ukiongozwa na wanawake wenye viriba tumbo na kupanda kutoka asilimia 29.7 hadi kufikia 31.7 ambao wapo katika hatari ya kupata magonjwa hayo yasiyoambukizwa.

Akifungua mdahalo huo, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, alisema licha ya Tanzania kujitosheleza na chakula kwa asilimia 120, lakini bado tatizo la lishe duni na udumavu bado ni changamoto kutokana na aina ya uzalishaji wa chakula katika maeneo husika.

Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Neema Shosho, alisema wadau wa maendeleo wanaipongeza serikali kwa jitihada zake za kutokomeza tatizo la utapiamlo na udumavu kwa watoto na kutaka kuongezwa kwa elimu juu ya namna ya mfumo wa maisha kwenye matumizi ya chakula.

Habari Kubwa