Chadema yafunguka Lissu kurejea nchini

14Oct 2019
Enock Charles
Nipashe
Chadema yafunguka Lissu kurejea nchini

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefunguka kuhusu usalama wa Mwanasheria Mkuu wake, Tundu Lissu, atakaporejea nchini kwa kueleza kuwa ni wajibu wa serikali kulinda raia wake.

Kutokana na hali hiyo, Chadema imeitaka serikali kutimiza wajibu huo kwa kuhakikisha Lissu anakuwa salama.

Akiongea na chombo kimojawapo cha habari nchini, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Itikadi na Uenezi ya chama hicho, John Mrema, amesema wanaunga mkono uamuzi wa Lissu wa kutorejea nchini mpaka kwanza ahakikishiwe usalama wake.

“Kama chama, tunaunga mkono kauli yake kwamba kwa sasa tunataka athibitishiwe usalama wake pindi atakaporudi, na wenye mamlaka ya kuhakikisha usalama wake ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu ni wajibu wa serikali kulinda usalama wa raia na mali zao,” alisema.

Akizungumza katika chombo kimojawapo cha habari cha kimataifa  wiki iliyopita, na kuulizwa  kuhusu mpango wake wa kurejea, Lissu alidai kuwepo kwa maneno katika mitandao ya kijamii yenye vitisho, hivyo kutishia  usalama wake endapo atarejea nchini.

“Wale walionipiga risasi 16 mchana wa saa saba katikati ya nyumba za serikali mjini Dodoma wakati wa kikao cha bunge bado wanaitwa watu wasiojulikana,” alisema Lissu.

Akizungumzia kuhusu maneno yanayojitokeza katika mitandao ya kijamii yenye viashiria vya vitisho kwa usalama wake, Lissu alidai kuwapo kwa vitisho vya wazi vya baadhi ya watu kuwa atakaporudi nchini watu hao watamshughulikia.

“Kuna maneno yanajitokeza tokeza kwenye hii mitandao ya kijamii kwamba ngoja aje mara hii hatutakosea shabaha… kuna aliyetangaza kwenye televisheni mtandaoni kwamba Lissu akija atapigwa risasi,” Lissu aliongeza.

Kuhusu hali yake ya kiafya Lissu alieleza kuwa ameshapona kabisa baada ya kukamilisha safari yake ndefu ya kimatibabu iliyoanza tangu Septemba 9 mwaka juzi jijini Dodoma na baadaye jijini Nairobi, Kenya na Ubelgiji alikokamilisha matibabu yake, hivyo kueleza kuwa sio sababu tena ya kuendelea kumuweka nje ya nchi.

Gazeti hili lilimtafuta Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, jana kuhusu madai ya Lissu na Chadema,  lakini simu yake haikupokelewa.

Hata hivyo, akizungumzia kuhusu usalama wa mwanasheria huyo wa Chadema miezi mitano iliyopita, IGP Sirro alisema kukurejea kwa Lissu kutasaidia kukamilisha uchunguzi na kufahamu waliohusika na shambulio lake, na kwamba kama raia wengine wa Tanzania, anahakikishiwa usalama wake kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. 

“Kwanza tunashukuru kuwa amepona na sasa anarejea, tutaweza

kufahamu zaidi waliohusika na shambulio lake, lakini pili usalama wake ni jambo la muhimu kama raia mwingine yeyote wa nchi hii ndio maana hata wewe upo salama kwa hiyo tutahakikisha anakuwa

salama,”   Sirro alisema.

Awali Lissu alipanga kurejea nchini Septemba 9, mwaka huu siku

ambayo mwaka 2017 alipigwa risasi 32 na watu wasiojulikana huku risasi 16 zikidaiwa kumpata mwilini, lakini baadaye aliahirisha kurudi kwa madai kuwa alikuwa hajamalizana na madaktari wake.

Hata hivyo Lissu aliahidi kuwa baada ya kuzungumza na madaktari wake Oktoba Mosi na Oktoba 8, mwaka huu angepanga tarehe nyingine ya kurejea nchini kabla ya kuahirisha tena wiki iliyopita safari hii akizungumzia hofu ya usalama wake.