Simba kuiteka Kigoma leo

14Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Simba kuiteka Kigoma leo
  • ***Aussems aichambua Mashujaa ilivyowatesa Kombe la FA, lakini asema hii ni timu... 

HUKU ikiwa imepata mapokezi makubwa baada ya kuwasili mkoani Kigoma jana asubuhi, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya "wababe wao" Mashujaa FC inayotarajiwa kuchezwa leo kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Mashabiki wa Simba kutoka sehemu mbalimbali mkoani humo, jana walijitokeza kuilaki timu hiyo kuanzia kwenye Uwanja wa Ndege, na kuisindikiza kwa magari, bajaj na pikipiki hali iliyofanya gari lililobeba wachezaji kupunguza mwendo.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Desemba 25, mwaka jana katika mchezo wa mashindano ya Kombe la FA Tanzania na Mashujaa inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ilifanikiwa kuiondoa Simba kwa penalti 3-2.

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems amesema mechi hiyo ya leo inaendelea kuwaimarisha wachezaji wake ambao walikosa nafasi za kuonyesha viwango vyao kwenye michezo minne ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyotangulia.

Aussems alisema amefurahi juzi kupata mchezo mzuri dhidi ya Bandari FC ya Kenya, hivyo anaamini leo pia kikosi chake kinatarajia kukutana na ushindani kutoka kwa wenyeji wao, Mashujaa.

"Najua haitakuwa mechi rahisi, tunakumbuka walitufunga mwaka jana, lakini hii ni timu nyingine na huu ni msimu mwingine, matumaini yangu ni kuona mechi nzuri na yenye burudani," alisema Aussems.

Kocha huyo aliongeza kuwa kila mechi husaidia kuimarisha sehemu fulani ya timu na ile inayoonekana kuwa na mapungufu, hufanyiwa kazi kwa ajili ya kufanya vema katika mchezo unaofuata.

Baada ya mechi hii, Simba itaendelea kubaki Kigoma na keshokutwa itawakaribisha Aigle Noir kutoka Burundi katika mchezo mwingine wa kirafiki utakaochezwa kwenye Uwanja huo huo kuanzia saa 10:00 jioni.

Ikirejea jijini, Simba itakutana na Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Oktoba 23, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa jijini. 

Habari Kubwa