Sababu uandikishaji daftari la mpiga kura kusuasua hii hapa

14Oct 2019
Dotto Lameck
Dar es Salaam
Nipashe
Sababu uandikishaji daftari la mpiga kura kusuasua hii hapa

ZOEZI la kujiandikisha katika daftari la wapiga kura limeonekana kuwa na muitikio mdogo katika baadhi ya maeneo mbalimbali nchini huku sababu kubwa ikielezwa kuwa ni elimu duni juu ya umuhimu wa kupiga kura pamoja na uhamasishaji.

Nipashe ilifanikiwa kuongea na baadhi ya mawakala wa vyama vya siasa kutoka sehemu tofauti, ambapo wameeleza utofauti wa muitikio wa watu kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na miaka iliyopita.

Said Kipati Wakala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) eneo la Temeke Jijini Dar es Salaam amesema katika eneo hilo muitikio wa watu kujiandikisha ni mdogo tofauti na walivyotarajia.

“Kwa mtazamo wangu sababu inayosababisha idadi ya watu kuja kujiandikisha kuwa ndogo ni elimu duni kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kupiga kura na sababu nyingine ni watu kuishi kwa mazoea, wanaona uchaguzi wa serikali za mitaa si muhimu” amesema Kipati.

Partick Mwambala wakala wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema muitikio katika eneo lake ni mzuri kiasi kuokana na wao kujitoa kuwaelewesha watu kwa kusimama barabarani kutokana na maandalizi hafifu.

“Muitikio katika eneo hili ni mzuri kiasi japo si kama ilivyozoeleka katika chaguzi zilizopita ila changamoto kubwa hapa ni maandalizi hafifu ya viashiria vya kuonyesha vituo vya kujiandikishia, hali ambayo inatulazimu sisi mawakala kusimama barabarani na kuwaelekeza watu kituo kilipo” amesema Mwambala.

Mtendaji wa mtaa wa Relini Kata ya Mtoni, Sepeku Mhina,ameeleza changamoto katika mtaa wake kuhusu muitikio wa wa uandikishaji ni uelewa mdogo kwa wananchi na kutojua vigezo vinavyohitajika huku wengi wakidhani kuwa kujiandikisha hadi uwe na kitambulisho.

“Sifa mojawapo ya kujiandikisha ni kuwa raia wa mtaa husika na kutimiza umri wa miaka 18 hakuna vitambulisho vinavohitajika, pia katika mtaa wangu tunahamasisha kwa kuwatumia wajumbe kupita katika nyumba anazoziongoza kuwahamasisha waje wapige kura kwa sababu ni haki yao ya msingi”

Mhina amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuacha usiasa na kudhani kuwa wanaotakiwa kujiandikisha ni  chama kimoja kwa sababu uchaguzi huu ni wa serikali za mitaa na lengo ni kuleta maeneleo katika mtaa husika.