Simba sasa yamaliza ushujaa wa Mashujaa

15Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Simba sasa yamaliza ushujaa wa Mashujaa
  • ***Shiboub na Ndemla wahitimisha kazi Aussems akiendeleza rekodi ya kutopoteza msimu huu huku...

PASI ndefu ya Hamisi Ndemla iliyomkuta Sharaf Shiboub na kuitendea haki kwa kuzamisha mpira nyavuni katika dakika ya 56, ilitosha kabisa kwa Simba kumaliza ushujaa wa Mashujaa katika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma jana.

Katika mechi hiyo ya kirafiki, Simba ilikuwa ikihitaji ushindi kwa namna yoyote ili kufuta hasira zake za kutolewa na Mashujaa katika michuano ya Kombe la Shirikisho maarufu FA Cup msimu uliopita baada ya kuchapwa mabao 3-2.

Mashujaa inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) msimu uliopita iliitoa Simba katika michuano hiyo, ikifuata nyayo ya timu nyingine inayomilikiwa na jeshi hilo, Green Warriors ambayo kabla ya msimu huo iliwatoa Wekundu wa Msimbazi hao kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya bao 1-1.

Kwa ushindi huo wa jana, kikosi hicho cha Mbelgeji Patrick Aussems kimeendelea kulinda rekodi yake ya kutopoteza mchezo wowote wa kimashindano na mechi za kirafiki msimu huu ikiwa ni baada ya Jumamosi iliyopita kuichapa Bandari FC ya Kenya kwenye mechi kali iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wakati huu wa mapumziko ya kupisha Kalenda ya Fifa, Simba imepanga kucheza mechi tatu za kirafiki kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Azam FC itakayopigwa Uwanja wa Taifa Oktoba 23, mwaka huu, hivyo itakamilisha ratiba hiyo kesho kwa kuvaana na Aigle Noir ya Burundi katika uwanja huo wa Lake Tanganyika.

Katika mechi ya jana, licha ya Simba kukabiliwa na changamoto ya ubovu wa uwanja, ilijitahidi kumiliki mpira lakini wachezaji walishindwa kuonyesha 'udambwidambwi' wao wa kuchezea mpira pamoja na pasi mpenyenzo hivyo mara nyingi kulazimika kutumia mipira ya juu.

Baada ya bao hilo la Shiboub, dakika ya 65 kama Ndemla angekuwa makini angeweza kuiandikia Simba bao la pili kufuatia kuachia mashine kali ya shuti lakini likapaa juu ya lango huku dakika ya 53, Rashid Juma alijaribu shuti lakini likawa chakula cha kipa.

Hata hivyo, dakika ya 85, Mashujaa walionana vema nje ya eneo la hatari la Simba, lakini walishindwa kuitumia nafasi hiyo baada ya Manula kuonyesha umahiri wake langoni kwa kucheza shuti lililoelekezwa langoni mwao.

Katika mechi hiyo ya jana Simba iliwaanzisha, Aishi Manula, Athuman Mtamilwa, Joseph Peter, Yusuph Mlipili, Kennedy Juma, Said Ndemla, Rashid Juma, Maulid Limbe, Dickson Mhilu, Ibrahim Ajibu na Francis Kahata.

Huku waliotokea benchi wakiwa ni Salum Shaban, Gerson Fraga, Sharaf Shiboub, Andrew Michael na Wilker Da Silva.