Elimu sasa ijielekeze zaidi kujitegemea

16Oct 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Elimu sasa ijielekeze zaidi kujitegemea

JUZI Oktoba 14 ilikuwa ni kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati, Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999, katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, jijini London, Uingereza.

Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo chake, watu wa kada mbalimbali wamemzungumzia kwa mapana na marefu Rais huyu wa kwanza wa Tanzania, kuhusu yale aliyofanya kwa ajili ya maendeleo ya taifa hili.

Binafsi ninaweza kusema kuwa kila elimu ya Tanzania inapozungumzwa siyo rahisi kumuweka pembeni Baba wa Taifa, kutokana na  ukweli kwamba siku zote alitamani kila Mtanzania apate elimu.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Baba wa Taifa alianza hilo mara tu baada ya nchi hii kupata uhuru, pale alipotangaza vita dhidi ya maadui watatu, maradhi, ujinga na umaskini.

Aliamini kwamba maadui wawili kati ya hao watatu, ambao ni umaskini na maradhi hawawezi kuondoka iwapo Watanzania hawatapata elimu.

Hivyo alifanya kila njia ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu bila kujali kama ni tajiri au maskini ili mradi tu awe ni raia mwenye akili timamu.

Kulikuwa na Azimio la Musoma la mwaka 1974 kuhusu watoto wote wenye umri wa kwenda shule wapelekwe huko ili wakapate elimu. Hii pia inaonyesha ni jinsi gani alitaka Watanzania wapate huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa na dunia kwa ujumla.

Hata watu wazima, ambao hawakubahatika kupata elimu rasmi, hawakuachwa nyuma, walikuwa na madarasa yao kila siku jioni baada ya kutoka kwenye shughuli za uzalishaji mali.

Jambo la kufurahisha ni kwamba elimu ilitolewa bure, hali ambayo kwa kweli wale ambao hawakuwa na matumaini ya kuipata kutokana na hali duni ya maisha, waliweza kuipata hadi ngazi ya chuo kikuu.

Baba wa Taifa alijikita zaidi kwenye elimu ya kujitegemea ili kuwajenga vijana kujifunza zaidi kazi za uzalishaji shuleni, na kuziwezesha shule zijitegemee kutokana na uzalishaji huo.

Muungwana anaamini kwamba juhudi za Baba wa Taifa za kutaka kila mtoto wa Kitanzania apate elimu zimerithiwa na serikali ya awamu ya tano, ambayo nayo imejikita katika hilo kwa kuruhusu watoto kusoma bure.

Serikali kuamua kubeba mzigo wa kulipa gharama zote kwa elimu ya msingi na sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne ni kuonyesha kwamba imedhamiria kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu.

Hatua hii ni wazi kwamba Baba wa Taifa anaenziwa kwa vitendo katika juhudi zake za kutaka Watanzania wote wanaelimika bila kuangalia uwezo wa mtu kifedha, bali wote kwake walikuwa sawa.

Muungwana anaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa ubunifu na weledi katika utendaji wake, lakini jambo la msingi zaidi ni kwamba ungefanywa mkakati ili elimu ijikite zaidi kwenye kujitegemea.

Mbali na kujitegemea, kazi hizo ziliwawezesha wanafunzi kujengwa kwa namna ambayo iliwapevusha fikra zao, na hivyo kuleta mtizamo chanya na mabadiliko ya kweli katika jamii kufuatana na ujuzi walioupata.

Hivyo juhudi za sasa za kutoa elimu bure pia zizingatie kuwajenga vijana wa Tanzania katika misingi ambayo iliachwa na Baba wa Taifa ambayo ni  elimu ya kujitegemea, watoto waelimishwe kuwa raia wa wema na wenye uzalendo.

Kwani nje ya wanafunzi kupewa elimu ya darasani, vilevile walipewa elimu ya stadi za maisha. Dhana hii ya Baba wa taifa aliyoiasisi juu ya elimu ya kujitegemea iliondoa mapungufu mengi yaliyokuwepo kwenye elimu ya mkoloni ambayo iliegemea zaidi katika jamii ya kibepari iliyooandaa watu kutawaliwa na si kujitawala.

Kimsingi unapozungumzia dhana ya elimu bure kuanzia elimu ya msingi mpaka kidato cha nne kwa sasa, hauwezi itenganisha na sera ya serikali juu ya elimu bure na pia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Habari Kubwa