Siku zilizoongezwa zitumieni kujisajili 

16Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Siku zilizoongezwa zitumieni kujisajili 

SERIKALI imeongeza siku tatu zaidi kwa ajili ya wananchi kujiandikisha ili waweze kupiga kura kuchagua viongozi wa vijiji, vitongoji, mitaa pamoja na wajumbe wengine.

Hii inamaanisha kuwa kesho ni mwisho wa kujisajili.

Tunaipongeza serikali kwa  kuona hitaji na umuhimu wa kuwaongezea muda ili kila mmoja ajiandikishe na kutumia haki yake kikatiba ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, vitongoji  na vijiji wanaofaa. 

Tunaungana na viongozi kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kwa sababu ili waweze kupiga kura na kumchagua mwenyekiti wa kijiji, kitongoji, mtaa  na wajumbe wa  serikali wanapaswa kujiandikisha kwanza kwani ndivyo matakwa na maelekezo ya kisheria.

Na sasa kwa wale ambao hawajajiandikisha ndiyo wakati wa kufanya hivyo ili kuwaweka madarakani viongozi watakaotuhudumia bila kutaka rushwa, kutunyanyasa na pia ni wakati wa kuwaondoa kwenye uongozi wale ambao ni wazembe na  wababaishaji na wasiowajibika.

Tunaungana na serikali kuwahimiza wananchi kujiandikisha ili kuchagua viongozi bora ambao watazishughulikia na kuzitatua kero za Watanzania katika ngazi za mwanzo  ikiwamo waliosababisha migogoro.

Tunawashauri wananchi wajitokeze na kujiandikisha kwa wingi ili kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa ambao watawaongoza kwenye masuala mbalimbali kama kuwapa utambulisho wa awali wakati wanafuatilia taarifa za kufungua akaunti benki.

Aidha, watakuwa wa kwanza kwenye kuwasaidia kwenye migogoro ya ardhi, kutatua matatizo ya kifamilia na usuluhishi kabla ya kwenda mahakamani.

Aidha, ni suala muhimu kushiriki wakifahamu kuwa hawa ndiyo watakaowaongoza kwa miaka mitano.

Tunaona kuwa kuna haja ya kuwachagua viongozi hawa kwani ndiyo wanaowajibika kufuatilia utekelezaji na uendelezaji wa mipango bora ya  maisha ya wananchi katika jamii zetu.

Hawa ndiyo wanaosimamia  na kushirikiana na wananchi kuleta mabadiliko chanya kwenye uzalishaji iwe kilimo, ufugaji, uvuvi na shughuli nyingine za maendeleo kwenye hatua za mwanzo.

Tukumbuke, kazi kubwa ya viongozi hawa ni kusimamia na kuendeleza ustawi wa jamii, kuhakikisha uwepo wa amani, utulivu, ulinzi, kuheshimiana na yote hayo  ili kuwe na jamii zilizo bora.

Kuchagua viongozi hawa ni muhimu kwani ndiyo wa kwanza kushughulikia matatizo ya wananchi katika hatua za mwanzo kwa ajili ya kutoa majawabu na ufumbuzi wa changamoto zao katika hatua za mwanzo.

Tukumbuke tunahitaji kuwa na viongozi hawa kwani ndiyo wa kwanza kujenga uhusiano wa uaminifu baina ya jamii na viongozi wao au wa serikali kuu.

Ikumbukwe kuwa iwapo watu hawatachagua viongozi bora, wakapuuza uchaguzi na wakawaachia wachache wakachagua wale wanaowapenda kwa maslahi yao, inaweza kusababisha wababaishaji hao kuingia madarakani, utakuwa  mwanzo wa kusababisha kufarakana baina ya watu na serikali.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa taswira ya serikali inaweza kuchafuliwa na viongozi wabovu na wasiowajibika wanaowachosha badala ya kuwahudumia wananchi.

Ndiyo maana tunaihamasisha jamii kufahamu kuwa kuchagua viongozi bora utakuwa ndiyo mwanzo wa kufahamu na kufuatilia masuala mbalimbali ya maendeleo yatakayoisaidia jamii katika kupata uelewa wa masuala muhimu ya maendeleo.

Wananchi tujitokeze kuchagua viongozi kwani hawa ndiyo wanaotuhamasisha kufahamu na kushiriki  masuala mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia taratibu, sheria na mifumo mbalimbali tuliyojiwekea.

Kwa msingi huo, tunawakumbusha wananchi kuwa kupiga kura lisiwe suala la hiari bali matakwa na maelekezo ya kikatiba.

Hivyo shime tutumie muda tuliongezewa kujiandikisha ili kupata viongozi bora na watakaotuhudumia kwenye ngazi za mitaa, vijiji na vitongoji.

Tusipuuze wajibu wa kujichagulia viongozi tushiriki na tuhakikishe kuwa tunawachagua walio bora kwa ajili ya maendeleo yetu.

Habari Kubwa