NMB yaja na mkopo rahisi kwa wateja

17Oct 2019
Allan lsack
MIRERANI
Nipashe
NMB yaja na mkopo rahisi kwa wateja

WAFANYAKAZI wa Benki ya NMB Tawi la Mirerani, Simanjiro mkoani Manyara, wamezindua Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kutangaza mpango mpya wa mikopo rahisi kwa wateja uitwao  ‘Afya Loan'. 

Meneja wa NMB Tawi la Mirerani, Allan Kombe, akizungumza juzi na wadau na wafanyakazi wa benki hiyo, alisema mkopo huo ni huduma mpya maalum ya watu au taasisi binafsi. 

Kombe alisema lengo la kuzinduliwa kwa mkopo huo ni kufungua milango ya kuwakopesha watu binafsi wenye maduka ya dawa, mashirika, taasisi binafsi, maabara, zahanati na vituo vya afya vya watu binafsi. 

Alisema ‘Afya Loan’ pia itaimarisha na kutoa  huduma  za afya zinazotolewa na watu binafsi au mashirika na taasisi binafsi. 

"Mpango huu utakuwa endelevu kwa wiki hii ya huduma kwa wateja itaendelea kwa muda wa mwezi mzima wa Oktoba," alisema Kombe. 

Ofisa Tarafa ya Moipo, Joseph Mtataiko, aliwapongeza wafanyakazi wa  NMB Tawi la Mirerani, kwa kutoa huduma vizuri kwa wateja pindi wanapofika kwenye benki hiyo.

Mtataiko alisema watumishi wa serikali, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji, wachimbaji madini na watu wa kada mbalimbali za Mirerani wanaopata huduma kwenye benki hiyo, kutokana na huduma nzuri zinazotolewa kwenye benki hiyo. 

Meneja wa Huduma kwa Wat    eja wa benki hiyo, Bahati Nelson, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau mbalimbali kufika kwenye ofisi za NMB kwa ajili kupatiwa huduma bora na za uhakika. 

Habari Kubwa