Madereva Bajaj sasa kushtakiwa 

17Oct 2019
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Madereva Bajaj sasa kushtakiwa 

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya, limewatahadharisha madereva wa Bajaj wanaokiuka sheria za usalama barabarani kuwa litaanza kuwashtaki mahakamani.

Waendesha Bajaj wakiwa wameegesha vyombo vyao nje ya ukumbi wa Mkapa, jana jijini Mbeya, walipofanya kikao na Jeshi la Polisi kuhusu mambo mbalimbali yakiwamo ya usalama barabarani. PICHA: NEBART MSOKWA

Akizungumza na madereva hao jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alisema wameamua kuacha kuwatoza faini madereva hao wanaokiuka sheria na badala yake wanawapeleka mahakamani.

Aliyataja baadhi ya makosa ya madereva wa bajaji ambayo yamekithiri kuwa ni kubeba abiria zaidi ya watatu, kuendesha bajaji bila leseni pamoja na kubeba mafuta ya petroli ndani ya vyombo hivyo licha ya kwamba wana abiria.

Kamanda Matei alisema mengine ni kuweka ngao kwenye bajaji hizo ambazo zinasababisha uharibifu wa vyombo vingine vya moto ikiwamo magari na pikipiki na hivyo akawaagiza kuziondoa kabla msako haujaanza.

"Mkuu wetu wa mkoa alikagua na kubaini kuwa zaidi ya asilimia 50 ya madereva wa bajaji hawana leseni, sasa ametuonyesha njia. Naomba kila anayeendesha vyombo hivi awe na leseni kabla hatujaanza msako," alisema Kamanda.

Vilevile alisema wamebaini kuwa baadhi ya madereva wa bajaji ni wadogo umri ambao hauwaruhusu kufanya kazi hiyo, hivyo akawatahadharisha wamiliki wa vyombo hivyo kuwa watachukuliwa hatua wao.Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bajaji wa Jiji la Mbeya, Iddy Ramadhani, aliliomba Jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana nao kupambana na matukio ya uhalifu likiwamo wizi wa vyombo hivyo.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakiiba bajaji katika maeneo mbalimbali nchini na kuzipeleka jijini Mbeya, kufanyia kazi ama kuziuza mkoani humo na hivyo kusababisha changamoto kubwa ya kiuhalifu.

Habari Kubwa