Tunapoitafakari Siku ya Chakula tuyatazame haya

17Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Tunapoitafakari Siku ya Chakula tuyatazame haya

OKTOBA ilikuwa ni Siku ya Chakula Duniani ambayo kwa mwaka huu inahimiza  umuhimu wa kuhakikisha lishe bora na endelevu inapatikana kwa wote na kwa gharama nafuu ili kuishi kwenye  dunia au kwa upande wetu kuwa na Tanzania isiyo na njaa.

Takwimu zinazotolewa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) zinaonyesha kuwa watu  wanakabiliwa na njaa, watoto mamilioni  wasichana kwa wavulana wenye miaka mitano  hadi 19 ni wanene wa kupindukia wakati mamilioni ya watoto chini ya miaka mitano  ni wazito waliopitiliza, lakini wapo mamilioni wenye udumavu wa kutisha.

FAO inasema walaji, hususan wa mijini hawana muda wa kutosha kuandaa vyakula nyumbani wengi wanakula chakula kutoka madukani au barabarani na kwenye migahawa na kwa ujumla wengi hutegemea chakula chenye wanga, sukari, mafuta, chumvi kwa wingi jambo linalotishia afya na ustawi wetu.

Kama ilivyo katika nchi kadhaa, Tanzania kwa upande mwingine nayo ina tatizo la watu kuwa na lishe duni inayosababishwa na milo ya watu kupungukiwa na viini lishe muhimu ambavyo vinahitajika na mwili kwa ajili ya afya njema au kusababishwa na ugonjwa, malezi na lishe mbovu ya utotoni, uchafu wa mazingira na ule wa mtu binafsi, kutofikia huduma za jamii na maji masafi. 

Nchi hii kama yalivyo mataifa mengine yenye uchumi unaokua, kuna shida ya ulaji ovyo unaoleta maradhi. Kila wakati magonjwa kama kuraha damu, kuharisha, taifodi na hata kipindupindu yamekuwa changamoto kutokana na ulaji ambao hauzingatii usafi katika kutayarisha vyakula mbalimbali hasa vinavyoandaliwa  mitaani na hata  nyumbani.

Aidha, tunaona kuwa kuna watu ambao hawana vibali vya kuuza vyakula lakini nao ni wajasiriamali ambao huhudumia walaji bila kujali usafi wala afya za watayarishaji hao. 

Kwa hiyo tuhamasishane kuwa kupata chakula chenye virutubisho muhimu na kilicho salama ndiyo ufunguo wa maisha na afya bora.

Kwa sababu tunalijua hilo ni wakati wa kuwahimiza Watanzania  kuacha kula vyakula visivyo salama vyenye bakteria na vimelea hatarishi na virusi pamoja na  kemikali nyingine.

Watu waanze kujiambia kuwa ni lazima  kuacha kula vyakula hivyo visivyo salama ambavyo  ni hatari kwa kuwa magonjwa zaidi ya 200 kuanzia ya tumbo hadi kansa hutokana na ulaji huo, kwa mujibu wa FAO.

Tukumbuke kuwa ulaji wa vyakula vyenye kemikali si lazima mwandaaji atume ‘sumu’ lakini ni mambo kama kutumia mafuta ya kukaangia chips, samaki au mihogo kwa muda mrefu bila kuyabadilisha.

Mathalani, waandaaji wengi huchuja mafuta hayo kwa  vitambaa na kuendelea kuyatumia muda wote au mwaka mzima bila kuyabadilisha. Hili ni  jambo linaloweza kuwa na athari kubwa kwa afya za binadamu japo hakuna utafiti uliofanywa kuujua ukweli.

Magonjwa yanayotokana na ulaji wa kemikali kama kulima na kumwagilia mboga majitaka ya viwandani nalo ni suala la kukemewa.

 Wapo wajasiriamali kwenye miji mingi ambao hulima na kuuza matunda na mboga yanayolimwa kwenye mazingira mabovu ambayo husambaza magonjwa kutokana na maji na ardhi inayotumiwa kwa kilimo kutokuwa salama.

Tukumbuke kuwa ulaji wa vyakula vyenye vimelea vya magonjwa, kama sambusa na mishikaki inayouzwa mitaani kutoka kwa ‘wamachinga wauza nyama’ vinavyouzwa sehemu mbalimbali kama shuleni na mitaani vinaweza pia kuwa chanzo cha magonjwa na vifo.

Ni hatari kwa sababu huenda nyama hizo hazijapimwa, nyingine zina kimeta na magonjwa ya mifugo.Hivyo tunapoadhimisha Siku ya  Chakula Duniani, tuhimize usafi wa vyakula kwa afya endelevu.