Kuchuja wanafunzi hakufai, wasiojiweza vyema wanolewe

17Oct 2019
Yasmine Protace
Mkuranga
Nipashe
Kuchuja wanafunzi hakufai, wasiojiweza vyema wanolewe

NI juzi tumesikia matokeo ya mtihani ya darasa la saba, mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiibuka kidedea kufanya vizuri kitaifa katika mitihani hiyo.

Pia, baadhi ya viongozi wa elimu katika mikoa hiyo wametoa ufafanuzi, kwamba ni matunda ya hatua kama kutoa vyakula shuleni, mitihani ya kila mara na mazingira bora ya elimu kwa jumla.Wanapaswa kupewa hongera.

Hiyo ni sura moja. Katika upande wa pili, kunaelezwa kuwapo shule hasa binafsi, ambazo katika kutafuta sifa kama zilizopatikana katika Kanda ya Ziwa mwaka huu, zina tabia ya kuwachuja baadhi ya wananfuzi, pindi wanaposhindwa kufikia wastani wa ufaulu walioupanga.

Kwa mtazamo wangu, kumuengua mwanafunzi asiyefanya vizuri katika mitihani au kumkwamisha, sio sababu ya kumaliza tatizo la ufaulu kwa wale wanaobaki.

Ikumbukwe, inawezekana hilo la kuenguliwa linaweza kuwakumba watoto waliokuwa na changamoto, hata alipofanya mitihani hawakuweza kufanya vizuri.

Kinachotakiwa hapo shuleni, ni kuhakikisha suala hilo wanalifanyia kazi, ili kuondoa malalamiko kwa wazazi.

Tunafahamu kuwa jukumu la mwalimu ni kuhakikisha wanawafundisha watoto waelewe na kufaulu zaidi madaraja walioko, wasonge kuelekea ngazi zaidi za juu kama vile vyuo vikuu.

Lakini kama walimu wataendelea kuwachuja watoto, wajue wao ndio watakuwa wamemfanya mtoto ashindwe kufikia malengo ya mbali na baadaye.

Hivi karibuni katika mahafali ya pamoja ya kidato cha nne katika shule za sekondari za Ujenzi,Victory, St.Mathew's na St. Mark's zilizoka Dar es  Salaam na Mkuranga, Pwani, mmiliki wa shule hizo, Peter Mutembei, anasema mfumo wao ni kutochuja wanafunzi kwa mujibu wa uwezo wao.

Anasema watoto walio na uwezo mdogo wanawapatia masomo ya ziada ili kuwafikia wenzao wenye uwezo mkubwa darasani na kwamba watoto wameweza kuwasaidia uwezo mdogo darasani na sasa wanafanya vizuri katika masomo.

Mutembei anaziasa shule ambazo zinazowachuja watoto ziache kufanya hivyo kwa sababu ni madaraja wanakoanzia watoto hao.

Naibu Waziri Ofis ya Rais (Tamisemi), Mwita Waitara, anasema suala la kuwachuja watoto ni kosa kwa sababu hata wazazi wanakuwa wameandaa fedha za ada kwa ajili ya watoto wao ndani ya kipindi maalum.

Waitara anasema, kinachotakiwa ni kutolewa elimu itakayowezesha kufikia mbali kimasomo na pindi mtoto anapojua ni dhana inayomuweka mzazi katika hatua ngumu.’

Pia, Waitara anasema wanatambua mchango unaotolewa na shule binafsi katika utoaji elimu, kwani umewasaidia baadhi ya wanafunzi wanakosa nafasi katika shule za serikali, wanakwenda kusoma katika shule binafsi.

Waitara anazitaka shule binafsi kuwachukua watoto wasio na uwezo kabisa na kuwaingiza katika shule zao, ili wapate elimu na kuna baadhi ya watoto ambao maisha yao ni magumu na hawakubahatika kupata elimu.

Habari Kubwa