Wakurugenzi ruksa kusimamia uchaguzi 

17Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wakurugenzi ruksa kusimamia uchaguzi 

MAHAKAMA ya Rufani Tanzania, imetengua uamuzi wa kesi iliyofunguliwa na Bob Wangwe katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, uliowazuia wakurugenzi wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi. 

Uamuzi huo ulitolewa juzi na jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani likiongozwa na Jaji Augustine Mwarija. Wengine katika jopo hilo ni Stella Mugasha, Richard Mziray, Rehema Mkuye na Jacobs Mwambegele.  

Kutokana na uamuzi huo, wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa na majiji kusimamia uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa miaka kadhaa iliyopita. 

Makahama Kuu katika uamuzi wake, kupitia kesi iliyofunguliwa na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, na wanaharakati  wa haki za binadamu, ilisema wakurugenzi hao kusimamia uchaguzi ni kinyume cha kifungu Na. 7 cha Sheria ya Uchaguzi.

Uamuzi wa Mahakama Kuu ilitolewa na jopo la majaji Dk. Atuganile Ngwala, Dk. Benhajj Masoud na Firmin Matogolo. 

Katika uamuzi wao, walikubaliana na hoja za mawakili wa mlalamikaji huku wakitolea mifano ya baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri ambao walishiriki kura za maoni ndani ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.    

Kwa mujibu wa jopo la majaji wa majaji hao, kitendo cha wakurugenzi hao, ambao baadhi yao ni wanachama wa vyama vya siasa, hususan Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinaifanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na uchaguzi mzima kutokuwa huru kwa mujibu wa Katiba. 

Jopo hilo la majaji wa Mahakama ya Rufani, katika uamuzi wake, lilikubaliana na madai ya serikali kupitia kwa Wakili wake Mkuu, Dk. Clemet Mashamba, kwamba wakurugenzi hao kabla ya kuwa wasimamizi, wanapaswa kula kiapo.

Katika kuwasilisha hoja zake, Dk. Mashamba alidai kuwa katika kutekeleza majukumu yao kama wasimamizi, wanawajibika kwa NEC ambayo ina mamlaka ya kuwaondoa iwapo watashindwa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa kiapo. 

Pia Dk. Mashamba alidai kuwa katika kiapo chao, wakurugenzi hao wanatoa tamko la kutokuwa na uhusiano na chama chochote cha siasa wanapotekeleza wajibu wao au wanajitoa uanachama wa vyama vya siasa. 

Katika uamuzi wake, jopo la majaji lilikubaliana na hoja hizo kwamba kiapo cha wakurugenzi hao na watumishi wengine wa umma kuwa wasimamizi wa uchaguzi, kinawaondoa kuwa na uhusiano au ufuasi wa chama chochote cha siasa.

“Wakurugenzi wanaweza kuwa walikuwa wanashiriki masuala ya kisiasa kabla ya kuteuliwa kushika nyadhifa hizo, lakini wanapoteuliwa na baadaye kuwa wasimamizi wa uchaguzi, moja kwa moja wanazuiwa kushiriki katika shughuli za kisiasa,” ilieleza sehemu ya hukumu hiyo. 

Habari Kubwa