Wananchi Chunya wahimizwa kujiandikisha Daftari la Wapiga kura

17Oct 2019
Kelvin Innocent
Chunya
Nipashe
Wananchi Chunya wahimizwa kujiandikisha Daftari la Wapiga kura

MKUU wa Wilaya ya Chunya Maryprisca Mahundi, amewaambia wananchi wa wilaya hiyo kuwa wasipojiandikisha watajuta ndani ya miaka mitano kwa kukosa maendeleo safi.

MKUU wa Wilaya ya Chunya Maryprisca Mahundi, picha mtandao

Mahundi amesema hayo alipokuwa akizungumza na wakazi wa wilaya hiyo na kusema serikali haiwatishi, lakini watajuta kwa sababu maendeleo huletwa na wananchi wenyewe hivyo wasipojiandikisha ni sawa nakujipa mzigo wao wenyewe.

“Msipo jiandikisha mtajuta ninamaanisha utajuta kwa miaka mitano na maendeleo yenu yatachelewa, unapoenda kujiandikisha hiko ndicho kichinjio chako," amesema Mahundi.

Aidha, Mahundi amesema kwamba lengo la Serikali kuongeza siku tatu za kujiandikisha ni kwa ajili ya kutoa haki za msingi kwa kila mwanachi.

Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha na kuwaondoa wasi wasi kuwa vitambulisho vya kupigia kura havita tumika katika uchaguzi wa 24, Novemba mwaka huu.

“Vitambulisho vya kupiga kura havita husika kwa hiyo ndiyo maana tunasisitiza ukajiandikishe na ukijiandikisha unakuwa mwananchi huru ambaye utaweza kupiga kura kwa kiongozi unaye mhitaji," amesema Mahundi.

Naye Mkuu wa Polisi Chunya OCD Emmanuel Bondo, amewataka wananchi wa wilaya hiyo ambao bado hawajajiandikisha wakajiandikishe na kutoa onyo kwa watakao leta vurugu katika uchaguzi huo.

“Nitoe onyo kwa watakaoleta kiherehere cha kufanya fujo kwenye vituo vya kupiga kura siku ya uchaguzi niwaonye wasijaribu na watakao jaribu moto watakao kutana nao siyo wakawaida," amesema Bondo.

Habari Kubwa