Wafanyabiashara waiangukia serikali

18Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wafanyabiashara waiangukia serikali

WAFANYABIASHARA mkoani Manyara  wamemwomba Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, awasaidie kufikisha kilio chao serikalini ili idadi kubwa ya taasisi za serikali zinazowabana kulipa kodi zipunguzwe   ama kodi zinazodaiwa ziunganishwe.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji

Lengo la ombi hilo ni kumwondolea mfanyabiashara adha ya kudhibitiwa na mamlaka nyingi.

Baadhi ya taasisi zilizotajwa ni Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) na nyingine ambazo wamesema mbali na kuwatoza kodi kubwa, lakini wamekuwa wakipata usumbufu wa aina mbalimbali.

Hata hivyo, wameahidi kuendelea kulipa kodi kwa hiari baada kuridhishwa na utendaji kazi wa serikali kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Walimweleza Dk. Kijaji aliyekutana nao Mjini Babati kujadili fursa na changamoto zinazoikabili sekta binafsi pamoja na kuwaelimisha namna serikali ilivyofuta kodi lukuki kwa lengo la kuwawezesha kufanyabiashara zao kwa tija zaidi.

Akijibu hoja mbalimbali za wafanyabiashara hao,  aliwapongeza kwa kulipa kodi ambayo imeiwezesha serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa vituo vya afya.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, Septemba, tumekusanya zaidi ya Sh. trilioni 1.76 kiasi ambacho hakijawahi kutokea tangu nchi ipate uhuru,” alisema Dk. Kijaji.

Alisema kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara ambapo mpaka sasa imeondoa zaidi ya kodi 50 zilizokuwa zikiwakwaza wafanyabiashara lengo likiwa ni kuwawezesha kufanyabiashara yao kwa ufanisi zaidi ili waendelee kulipa kodi.

“Tumepunguza kodi nyingi sana, mwaka wa fedha(2018/2019) tulipunguza kodi 108 na mwaka huu wa fedha (2019/2020) tumepunguza kodi na tozo 54 kwa makusudi, Rais John Magufuli ameamua kuwawezesha Watanzania, kila mmoja kwenye eneo lake la kazi afanye kazi vizuri,” alisisitiza.

Aidha, Dk. Kijaji aliwataka wafanyabiashara waliopata msamaha wa riba kwenye kodi mbalimbali walizokuwa wanadaiwa, walipe madeni yao kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na kwamba hakutakuwa na muda mwingine utakao ongezwa.

Aliwataarifu kwamba serikali imesitisha kwa muda utoaji fedha kwenye miradi mikubwa ya kimkakati iliyopangwa kutekelezwa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi yenye lengo la kuziwezesha halmashauri kujitegemea kimapato hadi pale mfumo madhubuti wa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo utakapowekwa.

Dk. Kijaji alitoa kauli hiyo baada ya kupokea maombi kutoka kwa Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul, aliyeomba Sh. bilioni 5.5 kutoka serikalini kwa ajili ya kujenga kituo cha mabasi ili kuboresha mazingira ya biashara na utoaji huduma kwa wananchi.

Naibu Kamishna Operesheni ya Kodi, Simon Kingu, alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iko tayari kushirikiana na wafanyabishara na kuhakikisha wanatatua kero zao ili walipekodi kwa hiari kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Habari Kubwa