Waziri aagiza hatua sakata kontena 38 chuma chakavu

18Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Waziri aagiza hatua sakata kontena 38 chuma chakavu

OFISI ya Makamu wa Rais imepokea ripoti ya uchunguzi wa kontena 38 za chuma chakavu zilizokuwa zisafirishwe nje.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene

Hata hivyo, kontena hizo zilizuiliwa bandarini Dar es Salaam. 

Ripoti imeeleza  kuwapo kwa udanganyifu mkubwa wa kusafirisha bidhaa  ambazo hazimo katika orodha ya vitu vilivyoruhusiwa kusafirishwa nje kama chuma chakavu au taka hatarishi.

Akipokea taarifa hiyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene, alisema  uchunguzi umeibua mambo mengi na kwamba serikali itawachukulia hatua kali wahusika wote katika kashfa hiyo.

“Ripoti inaonyesha kumekuwapo kwa hujuma kubwa ya miundombinu ya nchi; kwa mfano  mifuniko ya chemba za maji, nyaya za umeme, mataluma ya reli kinyume cha sheria na tarabitu za biashara ya chuma chakavu,” alisema na kuongeza:

“Ripoti imebaini hata kuwapo kwa kampuni isiyo na kibali cha kufanya biashara hiyo. Tutaifutia leseni ya biashara kampuni hiyo na nyingine zitakazoonekana zimefanya udanganyifu na kuuhujumu uchumi wa taifa.” 

Simbachawene alifanya  ziara katika   Bandari ya Dar es Salaam Agosti 9, mwaka huu.  Baada ya kuyaona kontena 38 za chuma chakavu zilizozuiliwa bandarini, alilagiza  Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamzi wa Mazingira(NEMC) kuwasilisha serikalini taarifa juu ya makontena hayo.

Alieleza kuwa katazo la serikali la kusafirishwa vyuma chakavu na taka hatarishi nje ya nchi limetokana na udanganyifu mkubwa wa wafanyabiashara.  ”Katazo hilo  lengo lake ni  kulinda viwanda vyetu  vinavyotegemea vyuma chakavu kama malighafi ya kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwamo nyaya za umeme na mikeka ya plastiki.”

Simbachawene alisema ni muhimu kulinda viwanda vilivyopo nchini kwa kuzuia malighafi kama chuma chakavu kusafirishwa nje ya nchi ili  kuongeza uzalishaji wa bidhaa na pia kuzalisha ajira nchini.“Ameeleza kuwa azma ya serikali ya ujenzi wa viwanda itafanikiwa iwapo kuna  malighafi kwa ajili ya viwanda vya ndani. 

Aidha, ametangaza kwamba kuanzia sasa hatoruhusiwa mtu yeyote  kukusanya, kuhifadhi, kusafirisha ama kupeleka kiwandani kwa ajili ya kurejeleza mali bila  kibali kutoka kwa waziri na kwamba mamlaka za serikali za mitaa ndizo zitakazosimamia ukusanyaji wa vyuma chakavu na taka hatarishi  kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja. 

Akiwasilisha ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, alieleza kuwa licha ya sheria kumtaka mfanyabiashara wa chuma chakavu kujaza fomu namba tatu inayoonyesha anakopata mali hiyo hakuna mfanyabiashara aliyefanya hivyo.

“Tutaendelea kusimamia sheria ili taratibu za kufanyabiashara zitekelezwe ikiwa ni pamoja na kuonyesha mzigo unakopatikana na kibali cha nchi ambako mzigo unakwenda,” aliahidi Dk.Gwamaka

Habari Kubwa