Tusipuuze chanjo tuwalinde watoto

18Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Tusipuuze chanjo tuwalinde watoto

MAMILIONI ya  watoto nchini wenye umri mbalimbali wanapewa chanjo kuanzia wiki hii hadi Oktoba 21. 

Ni sawa na kusema ni wiki ya chanjo ya kitaifa kwa watoto ambao kwa mujibu wa Wizara ya Afya watachanjwa surua, rubella  na polio.

Mamillioni ya watoto kote nchini watapokea chanjo dhidi ya magonjwa hayo  yanayowaathiri na wakati mwingine kusababisha vifo na ulemavu.

Chanjo hiyo iliyozinduliwa jana kitaifa mkoani Morogoro na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ni mojawapo ya njia za kuwaokoa watoto na magonjwa na kuwahikikishia kuwa wanalindwa ili wakue badala ya kufa wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano.

Ni vyema kujua kuwa maisha yao yanalindwa kutokana na magonjwa yanayoweza kuwaua, kudhibitiwa kupitia chanjo iwe kwa njia ya sindano au kuchanjwa.

Watanzania wanapaswa kujua kuwa chanjo ina tiba ya kuaminika na wataalamu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wanasema inaweza kuzuia vifo kati ya milioni mbili na tatu  kila mwaka.

Lakini, kwa upande mwingine Ripoti ya Shirika la Watoto la Kuhudumia Watoto (UNICEF)  inasema  mtoto mmoja kati ya watano  hajapata chanjo, hasa katika mataifa yanayokabiliwa na  migogoro ya kisiasa ikiwamo vita na uasi.

Ni wazi kuwa japo Tanzania hakuna uasi wala matatizo ya kisiasa, wapo   wanaopinga chanjo kwa madai kuwa inasababisha ugumba au kupunguza nguvu za kiume madai ambayo ni uzushi.

Kukataa chanjo kunaibuliwa na familia za watoto maskini ambazo mara nyingi zinakabiliwa na changamoto za kukosa huduma bora za afya kwa watoto kwani wana kipato cha chini na uwezo duni kiuchumi. Hali hiyo huchangia vifo vya watoto wao.

Hawa ndiyo wanaopinga chanjo na kutoa madai yenye uzushi. Wakati hayo yanazikuta familia maskini wale wenye uwezo wanawahudumia watoto wao kwa matababu, lishe bora  pamoja na chanjo na dawa nyingine za kutibu magonjwa. 

Ndiyo maana serikali inaleta ulinzi wa watoto kwa kutoa chanjo ili kuondoa au kupunguza tofauti hiyo ya kitabaka, kwa kuhakikisha kila mtoto anapata huduma bora za chanjo.

Kwa hiyo kila familia haina budi kumpa mtoto chanjo na kuachana na madai ya kizushi na uongo kuwa dawa hizo zina madhara hasa kupunguza nguvu za kiume na kuleta ugumba. 

Hebu wote tuone umuhimu wa  kila mmoja kuwajibika kuwachanja watoto  wengi bila kujali ni wafamilia maskini au tajiri ili watibiwe na kuwa afya bora kupitia chanjo.

Ikumbukwe hili si jukumu la serikali pekee kila mmoja anawajibika kuanzia mashirika ya kijamii na vyombo vya habari na  taasisi za dini ziunge mkono ili kusaidia kuiondoa jamii nyingi kutoka mila na tamaduni potofu ambazo hukataa au kupuuza manufaa ya chanjo hasa za vijijini na maeneo duni.

Ijulikane kuwa chanjo ni  kwa kila mtoto aliye na umri chini ya miaka 11 na ni  mkakati wa kuwalinda watoto wa Tanzania na vifo, magonjwa na athari nyingine zinazotokana na matatizo ya kiafya.

Hivyo tunaungana na serikali na wadau wengine kuhamasisha kampeni ya  kimataifa ya chanjo na kuwasihi wazazi, walezi, walimu na viongozi wa dini kuhakikisha kuwa utoaji  chanjo unafanikiwa.

Pamoja na hayo tunaomba viongozi wa serikali na jamii kupita nyumba kwa nyumba kuwabaini wale ambao hawajawachanja watoto na kuwaelimisha ila nao wawapeleke watoto wakapatiwe tiba hiyo inayowalinda na magonjwa kama kifua kikuu, surua, polio, homa ya ini na ndui.

Habari Kubwa