Kigogo sektabinafsi matatani

18Oct 2019
Dege Masoli
KOROGWE
Nipashe
Kigogo sektabinafsi matatani

MFANYABIASHARA nchini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta  Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte pamoja na  vigogo wa Kampuni ya Katan LTD, wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Tanga wakihusishwa na upotevu wa zaidi ya Sh. bilioni 54, zikiwamo za serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella

Kukamatwa vigogo hao ni agizo la Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella kwa Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Edward Bukombe na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa, Christopher Mariba.

Kamanda wa Bukombe aliwataja waliyokamatwa kwenye mkutano huo sambamba na Shamte ni Mkurugenzi Mtendaji wa Katan Ltd, Juma Shamte, Fadhil Mhina ambaye ni mhasibu wa Katan Ltd, Fatma Diwani mkurugenzi na Theodora Mtegeti Afisa mahusiano.

Shigela alitoa agizo hilo baada ya kupokea ripoti ya mkaguzi wa ndani

wa serikali aliyoitoa katika mkutano wa wadau wa mkonge uliofanyika jijini Tanga, ambapo ripoti hiyo ilionyesha kuwa Kampuni hiyo ina upotevu wa zaidi ya Sh. bilioni 54.

Awali akiwasilisha ripoti ya ukaguzi huo, Mkaguzi wa Ndani Mwaandamizi Wizara ya fedha na Mipango, Idrisa Ally, alieleza kuwa ukaguzi huo ulianza Januari 22, hadi Februaru 22 mwaka huu ambpo ulihusisha  mwaka 2008 hadi 2018.

Ally alieleza kuwa kazi ya ukaguzi huo ulilenga kuangalia miamala ya Shirika la wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wakulima na fedha za Sacos ya wakulima hao sambamba na kuangalia mikataba  iliyoingiwa na pande zote tatu.

Alieleza kuwa katika ukaguzi huo, zaidi ya Sh. bilioni 54 hazikufahamika zilipo ama matumizi yake yakiwamo madeni ya wakulima, makato ya wanachama wa NSSF, mkopo na kutolipwa kwa kodi ya serikali kwa mujibu wa taratibu.

Mkaguzi huyo alieleza yaliyojitokeza katika ukaguzi huo ni pamoja na madeni ya wakulima Sh. bilioni 29.8 ambazo hata hivyo alieleza hazikuonyeshwa kwenye taarifa za kampuni hiyo kiasi cha Sh. bilioni 1.7 za makato waliyokatwa wakulima huku Sacos ya wakulima ikiidai kampuni hiyo Sh. milioni  5.55.

Hata hivyo, ripoti ya mkaguzi huyo ilionyesha fedha zinazodaiwa na kampuni hiyo kwa wakulima ni zaidi ya Sh. bilioni 2.8.

Baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa kwenye mkutsano huo na Mkuu wa Mkoa kutoa nafasi kwa pande zote kujieleza ndipo Mmiliki wa kampuni ya Katan Ltd, Salum Shamte kusimama na kukanusha ripoti iliyowasilishwa hiyo akidai haina usahihi zaidi, na kwamba hawakushirikishwa katika kuiandaa.

Shamte alieleza kuwa wao kama walezi wa wakulima tangu mwaka 1999 walikuwa wakiendesha kilimo cha mkataba wa kibiashara baina yao,bodi ya mkonge na wakulima.

“Hakuna mkulima anaeibiwa kwani sisi zote lengo letu ni kuinua zao la mkonge kwa kuwanufaisha wakulima hivyo mheshimiwa mwenyekiti (RC) ripoti hii haikuhusisha walengwa yaani Katan Ltd, hivyo naomba ipitiwe upya kwa kushirikishwa,” alisisitiza Shamte.

 

 

Habari Kubwa