Tuegemee siri ya ufaulu kutoka Kanda ya Ziwa

18Oct 2019
Peter Orwa
Nipashe
Tuegemee siri ya ufaulu kutoka Kanda ya Ziwa

MATOKEO ya mtihani wa darasa la saba ambalo ndilo daraja la kumvusha mtoto kutoka elimu ya msingi kwenda sekondari, kwa wanaobahatika kuna maana kubwa, tangu yaanikwe hadharani .

Nikiwarejea wanafunzi, hilo ni jambo ninalolitamkia neno ‘bahati’ kwa maana wapo ambao kutokana na mitihani yao, kufaulu kumewahakikishia kuendelea na masomo tena bure. Sheria inawabana wazazi kuwajibikia hilo, ama watake au wastitake watoto hao wanandelea na sekondari.

Mbali na hilo, mahali hapo hakuna gharama zozote, cha muhimu kwao nikujitoa kitaaluma ili kufanikisha lengo.

Pia, kuna lingine la wale walau wana ahueni kiuchumi. Daima wanahakikishiwa kuendelea na masomo ya sekondari katika shule binafsi iwe wamefaulu au la.

Wapo ambao sura yao katika tija ya kitaaluma. Nao huwa zaidi wanapatikana katika shule za sekondari za kulipia.

Jambo ninalotaka kusema ni kwamba, katika matokeo hayo ya wiki hii kuna mengi ya kujifunza ambayo mazuri yanaweza kusambazwa kutumika kila mahali na mabaya yakakandamizwa.

Ukanda wa Ziwa ndio umekuwa kinara katika kiwango cha ufaulu. Ni kiasi gani kanda nyingine za nchi zinaweza kudodosa hayo kunusa siri ya tija.

Kuna asasi huru za kitaaluma nazo zimedokeza mambo kadhaa ya kitaaluma. Zote zikikusanywa na kuwekwa sehemu moja inazaa makubwa katika maamuzi ya jumla.

Hatuishii hapo, kwani matumizi ya elimu yanafika mbali zaidi ya manufaa ya mitihani. Elimu ni dhana inayotafsiri makubwa zaidi, maisha halisi ya jana, sasa na baadaye. Inabuni na kutafsiri njia ya maisha.

Msingi bora unawekwa katika elimu kuanzia ngazi ya chini, inasaidia ubora hadi ngazi ya juu zaidi kutoka hapo tulipo.

Mwanafunzi anapojiunga na masomo ya vyuo, iwe kunakotolewa digirii au vyeti vingine vya kati na maarifa ya jumla wa elimu inampa msingi bora mhusika.

Mwanazuoni wa chuo, awe mkufunzi au mhadhiri wote ufanisi na mafanikio ya kazi yake katika kutoa elimu inaanzia katika tija ya uelimishaji inayotolewa chini msomaji huyo alikotokea.

Tija ya msomaji si cheti pekee. La hasha! Inaenda mbali kidogo katika wasifu kama kiwango cha uelewa, mbinu za usomaji na nidhamu ya usomaji wake.

Hiyo ndiyo inayorejesha mkasa katika chuo fulani cha elimu ya juu kukumbwa na vichekesho ndani ya ulingo wa mjadala wao wa kitaaluma, kilio kikuu kikiangukia katika madhara ya kuendekeza tuisheni, badala ya mwanafunzi kujikita rasmi katika usomaji.

Inafahamika tuisheni stadi tegemezi inayomtoa nje ya mstari msomaji akikaririshwa mambo ambayo anaweza kuyabandika katika majibu ya mtihani na hata akafaulu, lakini akibanwa  kuonyesha wigo wa uelewa anaagukia katika ‘sifuri.’

Mtaaluma mmoja wa sosholojia alitoa ushahidi wa kilichomkuta, akiungwa mkono na mwenziwe mwanasheria, wote wakijenga hoja kwamba walipatwa na mshangao.

Huo ulihusu mwanachuo wa darasa la ngazi yao, katika matukio mawili tofauti wakidai darasa la tuisheni na mambo yanayofanana nayo. Ilikuwa aibu!

Je cha kujiuliza, kosa limeegemea mahali gani? Hapo ana shaka ni huko katika ngazi chini ambako kuna msingi.

Swali zaidi laweza kujitokeza, kulikoni yakatokea leo na zamani hayakuwako?  Nani anawajibika nao hilo? Kunawezekana kukawepo maswali mengi, yenye majibu ya kigugumizi.

Hapo ndipo dhana kukumbatia ufafanuzi wa mikoa Kanda ya Ziwa na siri yao ya ushindi katika mahali penye msingi wa elimu. Walishadokeza kadhaa kama mlo wa mchana.

Habari Kubwa