Yanga isake magoli  kuivuruga Pyramids

21Oct 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Yanga isake magoli  kuivuruga Pyramids

YANGA itacheza mechi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids kutoka Misri kwenye mechi ya mkondo wa kwanza, hatua ya mtoano, kabla ya timu hizo kurudiana baada ya wiki moja.

Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambako viongozi wa Yanga wameamua waipeleke kwa sababu mbalimbali walizoanisha.

Ni mechi ambayo timu yoyote ikifanikiwa kupata matokeo mazuri kwenye mechi zote mbili za nyumbani na ugenini, basi itatinga moja kwa moja kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga iliingia hatua hii baada ya ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Zesco ya Zambia, huku Pyramids ikiwa kwenye michuano hii tangu mwanzo.

Ni ukweli usiopingika kuwa ni mechi ngumu kwa wawakilishi hao wa Tanzania, kwani rekodi inaonyesha kwamba timu za Afrika Kaskazini maarufu kama timu za Waarabu huwa zinazisumbua sana timu za Tanzania, lakini Yanga yenyewe imekuwa haina bahati ikikutana na timu za Waarabu kwenye michuano hii mikubwa barani Afrika.

Katika mechi hii ili Yanga ifanye vema, kwanza kabisa ni lazima benchi la ufundi lifanye kazi yake sawasawa na lisiwaaminishe wachezaji kuwa kwa sababu mechi imehamishiwa Mwanza, basi itashinda kirahisi.

Ni lazima machozi, jasho na damu vimwagike kwa pamoja ili kupata ushindi kwenye mechi hiyo, kwa nia moja tu ya kuhakikisha inajiweka vema kwenye mechi ya marudiano ambayo itakuwa ngumu zaidi kuliko hata ya Kirumba.

Wachezaji wa Yanga wacheze soka la kushambulia zaidi kusaka magoli na si kudhani kuwa huwa hawawezi kushinda nyumbani, badala yake hushinda ugenini. Siyo kila siku Ijumaa. Tumeona ilivyotokea nchini Zambia. Na ni ngumu zaidi kushinda nchini Misri, tena kwa idadi kubwa ya magoli.

Kwa maana hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, awatengeneze vijana wake wacheze soka la kushambulia muda wote kwa ajili ya kusaka idadi kubwa ya magoli.

Nimeona baadhi ya mechi za Yanga, pamoja na kwamba wana matatizo kwenye nafasi ya ushambuliaji, lakini hata mfumo wenyewe wanaocheza huwa ni wa kujilinda, iwe kwenye Ligi ya Mabingwa au kwenye Ligi Kuu.

Kwenye mechi dhidi ya Coastal Union, Yanga baada ya kupata bao moja, ilionekana kujilinda zaidi kuliko kushambulia, kitu ambacho si cha kawaida sana kwa timu kubwa kama hiyo kujilinda dhidi ya timu ndogo, badala ya kusaka bao la pili.

Mfumo wa kujilinda ndiyo ulioiponza timu hiyo kwenye mechi dhidi ya Zesco, kwenye mechi zote mbili ya Dar es Salaam na ugenini. Wakati ikilinda ushindi wa bao moja, ilijikuta ikisawazishiwa bao dakika za majeruhi nyumbani na wakati ikijilinda ikidhani itakwenda kwenye mikwaju ya penalti, ilijikuta ikichapwa bao la pili ugenini.

Bao 1-0 pekee kwenye mechi dhidi ya Pyramids halitoshi, badala yake Yanga inatakiwa ifunge magoli kuanzia mawili na kuendelea, huku isiruhusu wavu wake kuguswa.

Hapo inaweza kujiweka kwenye mazingira ya kuwapa presha wapinzani wao kwenye mechi ya marudiano, vinginevyo hali inaweza kuwa mbaya. 

Tunawatakia kila la kheri Yanga, wawakilishi pekee wa Tanzania, waliobakia kwenye michuano hiyo ya kimataifa inayofanyika kila mwaka.

Habari Kubwa