Majaliwa aibana mikoa agizo uwekezaji

21Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa aibana mikoa agizo uwekezaji

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameitaka mikoa ambayo bado haijatekeleza agizo lake la kuandaa makongamano ya uwekezaji ihakikishe inafanya hivyo mara moja.

Ametoa agizo hilo leo mchana wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji kwa mkoa wa Pwani katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza viongozi wa mkoa wa Pwani kwa kutekeleza agizo nililolitoa Juni 18, 2018, wakati wa kongamano la tatu la uwezeshaji wananchi kiuchumi la kuhakikisha mikoa yote inaandaa kongamano la uwekezaji na inakuwa na mwongozo wa uwekezaji wa mkoa. Mikoa ambayo haijatekeleza agizo hilo, ifanye hivyo mara moja,” amesema.

Alisema mkoa huo umeweza kubaini fursa zilizopo katika mkoa wa Pwani na kuzitangaza kupitia mwongozo wa uwekezaji ambao pia ulizindulia juzi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe wanasimamia miundombinu inayoelekea kwenye viwanda vilivyopo kwenye maeneo yao.

"Kila mmoja ahakikishe maji, umeme na barabara vinafika kila eneo ambalo mwekezaji anataka kujenga kiwanda. Nitumie fursa hii kuwaomba mlete mabadiliko chanya yanayotokana na maboresho yanayofanywa na serikali.”

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angella Kairuki, alisema serikali imeanza kutekeleza mapendekezo ya mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa kuondoa tozo 163 zilizokuwa zikilalamikiwa na wawekezaji.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikillo, aliwataka watu wote wanaotaka kuwekeza nchini waufikirie kwanza mkoa wa Pwani kwa sababu uko kimkakati na una fursa nyingi ikiwamo hali nzuri ya usalama na kwa maana hiyo mitaji yao italindwa.

“Mkoa wetu uko kwenye eneo la kimkakati la kuwezesha biashara kwa kuwa uko karibu na Bandari ya Dar es Salaam na uwanja wa ndege; uko karibu na soko kubwa ambalo ni Dar es Salaam; unapitiwa na reli zote kwenda mikoani na nchi jirani; unapitiwa na barabara kuu itokayo Dar es Salaam na pia una bandari kavu ya Kwala.”

Dk. Tausi Kida, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchumi ya Kijamii (ESRF) ambayo ilisimamia uandaaji wa mwongozo wa uwekezaji kwa mkoa wa Pwani, alisema taasisi yao inasaidia kuandaa na kuchambua fursa zilizopo kwenye mikoa mbalimbali.  “Hadi sasa tumekwishaisaidia mikoa 17 kuandaa miongozo ya uwekezaji na kwa sasa mikoa 12 imeshakamilisha na mikoa mitano iko kwenye hatua mbalimbali,” alisema.

Akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, ambao ni wadhamini wakuu, Ofisa Mkuu wa Biashara, Benki ya CRDB, Dk. Joseph Witts alisema:

“Benki yetu inatoa mikopo ya biashara na uwekezaji katika maeneo mbalimbali ambapo mikopo ya kilimo ni Sh. bilioni 357, uzalishaji wa viwanda (Sh. bilioni 214), biashara (Sh. bilioni 347), hoteli (Sh. bilioni 87) na sekta ya madini (Sh. bilioni 91),” alisema.

Habari Kubwa