RC Mnyeti aridhishwa na utekelezaji wa miradi

21Oct 2019
Allan lsack
MANYARA
Nipashe
RC Mnyeti aridhishwa na utekelezaji wa miradi

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, amefurahishwa na kasi ya wananchi wa kata za Bwawani na Matui kwa  usimamizi mzuri wa fedha za serikali katika ujenzi wa madarasa ya shule wilayani Kiteto.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti

Akiwa katika ziara yake ya kikazi kukagua miradi na kutatua changamoto wilayani humo, Mnyeti alitembelea ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu alisema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na matumizi ya fedha.

Alisema ujenzi wa madarasa pamoja na nyumba za walimu ulitekelezwa katika vijiji vya  Bwawani, Kazingumu na Azimio na kila kijiji kilipokea fedha kiasi cha Sh. milioni 60, kutoka kwa  mamlaka ya elimu Tanzania (TEA), kwa ajili ya kutatua changamoto ya upungufu wa madarasa.  

Shule zilizopokea fedha hizo, ni Shule ya Msingi Kazimu na Azimio, ambapo shule ya msingi Azimio ilipokea kiasi cha Sh. milioni 60, kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na nyumba moja ya walimu.

Shule ya Kazingum ilipewa  fedha Sh. milioni 66, kutoka kwenye programu ya elimu bila malipo (EP4R). 

Fedha hizo, zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa  na matundu sita ya vyoo,  na katika Shule ya Msingi Bwawani walijenga  ofisi moja ya walimu na matundu 12 ya vyoo na vyumba vitatu vya madarasa na ilipokea Sh. milioni 60.

"Niwapongeze kwa kujenga miundombinu mizuri  ya gharama nafuu kwa kutumia Sh. milioni 12, kwa kila darasa na tayari madarasa yamekamilika na umeme umewekwa pamoja na gypsum  kupitia fedha hizi, sehemu nyingine ujenzi huu umetekelezwa kwa gharama ya kiasi cha Sh. milioni 17, kwa kila darasa moja na bado haukukamilika," alisema Mnyeti. 

"Tumetembelea maeneo mengine wametumia Sh. milioni 60, kujenga madarasa mawili na fedha zimeisha bila  ujenzi kukamilika, watu waliokula fedha hizo tunavyoongea watu hao wapo magereza,” alisema Mnyeti.

Alisema serikali itaendelea kuunga mkono maeneo ambayo watakuwa na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo huku akiwataka wananchi kuongeza nguvu kwenye miradi hiyo kwa kuchangia fedha pale zinapohitajika na siyo kutengemea fedha za serikali peke yake. 

Mwalimu Mkuu wa Shule ya  Azimio,  Johnson Shirima, alisema  kukamilika kwa mradi huo kumesaidia wanafunzi na walimu kupata eneo la kufundishia na kujifunzia lakini pia vyumba vya madarasa vilivyojengwa vimepunguza  changamoto ya msongamano wa wanafunzi  uliokuwapo mwanzo.