Maandalizi kuelekea fainali CHAN yaanze 

21Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Maandalizi kuelekea fainali CHAN yaanze 

KWANZA kabisa gazeti hili linapenda kuipongeza Timu ya Taifa (Taifa Stars), benchi la ufundi na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kufanikiwa kupata tiketi ya kushiriki katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Ilikuwa ni Ijumaa ya Oktoba 18, mwaka huu, kwa wachezaji wa Taifa Stars kuweka rekodi nyingine kwa nchi baada ya kufanikiwa kukata tiketi ya kushiriki fainali hizo za CHAN.

Hii ni mara ya pili kwa Taifa Stars kufuzu kushiriki fainali hizo. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2008, fainali zilichezwa mjini Abdijan, Ivory Coast na kikosi hicho kilikuwa chini ya Mbrazil Marcio Maximo.

Taifa Stars ambayo sasa iko chini ya Mrundi Etienne Ndayiragije, imefuzu kushiriki fainali hizo baada ya miaka 10, tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza.

Ukionekana kuwa mwaka wa neema kwa Watanzania, mwaka huu pia, Taifa Stars, ilifanikiwa kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019), ikiwa imekaa nje ya michuano hiyo kwa miaka 39.

Hiyo ilikuwa ni historia, sasa ni wakati wa kuanza maandalizi kuelekea fainali hizo ambazo zitachezwa Februari, katika miji ambayo itajulikana hapo baadaye.

Februari sio mbali, huu ndio wakati sahihi kwa TFF kuanza kuiandaa timu hiyo ili iweze kwenda katika fainali hizo ikiwa imara.

Si vema Watanzania tukashuhudia timu yetu inapoteza mechi zote za hatua ya makundi, hali ya kuwa muda wa kujiimarisha na kujiweka sawa upo.

Licha ya kukabiliwa na ratiba ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, si jambo baya kama idara ya ufundi itaamua kuangalia nchi nyingine zinavyojipanga, kwa maana ya kuona kikosi cha Taifa Stars kinapata muda wa kukutana na kujifua na vile vile mechi za ligi zikiendelea bila kuwapo kwa malalamiko.

Inawezekana jiografia ya Tanzania inakuwa ni kikwazo, lakini hakuna jambo linaloshindikana kama serikali, ambao ndio wadau wakuu, taasisi na kampuni mbalimbali kukajitokeza kuidhamini timu hiyo kwa lengo la kuhakikisha inakuwa imara na inakwenda kuonyesha ushindani huko Cameroon.

Nipashe tunaamini kuwa mchezo wa soka hauhitaji miujiza, timu inayojiandaa vema ndiyo inayojiweka kwenye nafasi ya kufanya vizuri katika fainali hizo na si kutegemea miujuza.

Siku zote tunakumbushwa kuwa mambo mazuri hutokana na maandalizi sahihi, kuwekeza kuanzia kwenye maandalizi, ndio jambo sahihi na kamwe tuache kusubiri mafanikio au kutoa ahadi za zawadi kwa mchezaji atakayefunga bao, au timu itakapopata matokeo chanya.

Kuwekeza katika maandalizi, kutawafanya wachezaji watakaokwenda katika fainali za CHAN kuwa na viwango bora, na hiyo itaonekana kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara ambayo ndiyo inatoa idadi kubwa ya nyota watakaokwenda kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano hiyo.

Endapo Taifa Stars, itafanya vizuri katika fainali hizo, ina maana wachezaji wengi wa Tanzania watapata timu za nje na watakaporejea, wataisaidia timu hiyo kufanya vema.

Lakini, walengwa ambao ni wachezaji na wanafaidika moja kwa moja, wanatakiwa kujipangia programu zao binafsi ili kuendelea kukuza vipaji vyao.

Kama Algeria na Senegal, ziliweza kufanya vizuri katika fainali zilizopita za Afcon, basi na Tanzania inaweza kufika katika mafanikio hayo, endapo tu, wadau wote watakubali kuwekeza katika mchezo huo, kuanzia ngazi ya watoto na vijana.

Habari Kubwa