Vipodozi 16 vyaondolewa madukani Dar

21Oct 2019
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam.
Nipashe
Vipodozi 16 vyaondolewa madukani Dar

MAOFISA wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wamefanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye maduka ya vipodozi na kuondoa aina 16 za vipodozi vilivyopigwa marufuku kwa matumizi ya binadamu.

Vipodozi vilivyoondolewa kwenye soko vinaelezwa kuwa na viambata vyenye sumu hivyo kuhatarisha afya kwa watumiaji.

Maofisa hao walifanya ukaguzi huo mwishoni mwa wiki kwenye maduka mbalimbali yaliyopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ukaguzi huo, Mkaguzi Mwandamizi wa Shirika hilo, Mhandisi Donald Manyama, alisema wauzaji wa vipodozi hivyo wameonyesha ushirikiano wa kutosha kwani wamevitoa kwa kadri ambavyo walielekezwa.

Alipoulizwa kama kuingia nchini kwa vipodozi hivyo, kunachangiwa na kutokuwapo udhibiti wa kutosha mipakani, Mhandisi Manyama alisema udhibiti upo wa kutosha, lakini vitu ambavyo vimepigwa marufuku nchini vinaingia kwa njia ambazo siyo halali.

Alisema waingizaji wamekuwa wakitumia njia za panya kuingiza vipodozi hivyo na kwamba vile walivyonikamata wamevichukua kwa ajili ya kwenda kuviharibu.

"Operesheni hiyo siyo kwamba itaishia hapa Dar es Salaam, baada ya kumaliza hapa tutaendelea na ratiba yetu mikoani kuondoa vipodozi hivi," alisema Mhandisi Manyama.

Kuhusu madhara ya vipodozi hivyo vyenye viambata sumu kwa matumizi ya binadamu, alisema vina madhara kwenye ngozi ya binadamu.

"Kwanza vinaichubua ngozi na kuifanya kuwa laini kiasi kwamba mtumiaji akifanyiwa operesheni ushonaji wake unakuwa ni mgumu," alisema na kuongeza;

"Vingine vinasababisha saratani, hivyo tunawashauri hata watumiaji kuacha kutumia vipodozi hivyo. Wengine wanavitumia bila kufahamu wakiona mwenzao amebadilika ngozi wanadhani havina madhara,” alisema.

Alisema wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waache kutumia vipodozi hivyo na alitoa wito kwa wasambazaji wa vipodozi hivyo kuacha kwani wakikamatwa mitaji yao itapotea na watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kutozwa faini.

Baadhi ya vipodozi vilivyokamatwa kwenye ukaguzi huo na kuondolewa sokoni ni Carolight, Movate, Coco Pulp, Diproson,Viva White, Carotone, Bronz na Eclair.

Vingine ni Citrolight, Tent Clear, Tender White, Clinic Clear, TCD, Baby Face, Light up, Dermotyl na Top Lemon. 

Mmoja wa wauzaji wa vipodozi hivyo, Rose Joseph, alishauri udhibiti uimarishwe zaidi mipakani kwani kama vitaendelea kupatikana vitazidi kupata soko.

Habari Kubwa