VAR kutumika  Simba vs Yanga

21Oct 2019
Isaac Kijoti
Dar es Salaam
Nipashe
VAR kutumika  Simba vs Yanga
  • ***TFF yapanga kumaliza utata wa waamuzi katika mechi hiyo, yateta na Wachina kuja... 

KWA mara ya kwanza katika historia ya soka la Tanzania kama si Afrika Mashariki kwa ujumla, Watanzania wanaweza kushuhudia Teknolojia ya Video ya Kumsaidia Refa (VAR) ikitumika nchini kwenye mechi ya Simba na Yanga. 

Ili kuondoa lawama na shutuma kwa mwamuzi ambazo zimekuwa zikijitokeza katika mechi ya watani hao wa jadi, Shirikisho la Soka nchini (TFF), lipo katika mchakato wa kuhakikisha VAR inatumika katika mechi mbili Simba na Yanga zitakapokutana. 

Akizungumza katika mkutano wa wahariri wa michezo wa vyombo mbalimbali vya habari nchini uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, alisema wapo katika mazungumzo na wataalamu wa teknolojia hiyo kutoka barani Asia. 

Kidao alisema tayari wamezigusia klabu husika, Simba na Yanga kuhusu mpango huo na kwamba pamejitokeza mvutano kidogo ila wanaendelea kujadiliana. 

"Tulipokuwa katika mkutano wa Caf (Shirikisho la Soka Afrika) tulikutana na wahusika tukazungumza nao na kututajia gharama kwa mechi moja ni Dola za Marekani 4,500 (zaidi ya Sh. milioni 10 za Tanzania).

"Ni gharama ambazo tunaweza kuzimudu ili kuleta ufanisi na zaidi kuondoa lawama na shutuma zilizozoeleka kwa waamuzi zinapokutana timu hizo," alisema Kidao.

Alisema pamoja na kutaka kushughulikia mchakato huo viongozi wa klabu hizo wamegawanyika huku baadhi wakionekana kuukubali na wengine wakipinga. 

"Pamoja na nia yetu nzuri bado kuna baadhi ya viongozi wa klabu hizo hawataki VAR itumike ila kwa sababu muda bado upo tunaweza kukubaliana," alisema. 

Mechi ya raundi ya kwanza itakayoikutanisha miamba hiyo Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam inatarajiwa kuchezwa mapema Januari mwakani.

Katika mkutano huo ambao TFF ilikuwa ikieleza mafanikio yake ya miaka miwili chini ya Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia, mbali ya wahariri wa michezo, pia ulihudhiriwa na wadau mbalimbali wa soka. 

Aidha, Karia mbali ya kueleza mafanikio mbalimbali waliyoyapata ikiwa ni pamoja Taifa Stars kufuzu na kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) nchini Misri na zile za Wachezaji wa Ndani (CHAN) mwakani nchini Cameroon,  alisema wamepata wawekezaji mbalimbali waliomba kujenga akademi za soka hapa nchini.

"Kuna wawekezaji kutoka yalipo makao makuu ya soka duniani, Uswisi na wengine kutoka Misri wameomba wapewe eneo la kujenga akademi za soka nchini. 

"Hawa wa Uswisi tayari wameonyeshwa eneo Dodoma na hawa wa Misri tunawatafutia hapa Dar es Salaam," alisema Karia. 

Habari Kubwa