Nchimbi: Nilijua  nitaifunga Sudan

21Oct 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Nchimbi: Nilijua  nitaifunga Sudan

MSHAMBULIAJI wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) na klabu ya Polisi Tanzania, Ditram Nchimbi, amesema kuwa alijiandaa kufunga goli katika mechi dhidi ya Sudan, lakini furaha yake imeongezeka zaidi baada ya kufunga bao muhimu katika mchezo huo.

Nchimbi ambaye aliitwa kuchukua nafasi ya nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, aliyekuwa na udhuru kuelekea mechi ya kirafiki dhidi ya Rwanda, alifunga bao la ushindi ambalo limeipeleka Tanzania kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Akizungumza na gazeti hili, Nchimbi, alisema kuwa lengo lake la kupambana kuhakikisha anafunga, lilikuwa ni kudhihirisha uwezo wake na kutomwangusha Kocha Etienne Ndayiragije ambaye alimwamini na kumpa nafasi hiyo kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho.

Nchimbi alisema pia mbali na kujipanga kuivusha Stars, aliamini mechi hiyo dhidi ya Sudan ni mwanzo wa kusaka timu nje ya Tanzania.

"Nilijua nitafunga, nilikuwa na ndoto hizo, tangu jina langu lilipojumuishwa katika kikosi cha Stars, nikawa ninajipanga kukahikisha ninafanya kile ninachokiwanza, lakini kikubwa nilijuwa itakuwa ni bao la kuanzisha safari yangu ya kucheza soka Ulaya," alisema Nchimbi.

Aliongeza kuwa atahakikisha analinda kiwango chake, ili itakapofika fainali hizo za CHAN hapo mwakani, awe ni mmoja wa wachezaji watakaokwenda kupeperusha bendera ya Tanzania katika michuano hiyo.

"Nimeshaingia kwenye rekodi, ninajua kila mmoja atakuwa ananifuatilia, nitajituma kuhakikisha ninaendelea kufanya vema katika kila mchezo, nitakapopata nafasi, naamini wachezaji wenye vipaji ni wengi, lakini nafasi huwa chache," Nchimbi aliongeza.

Bao la kwanza katika mchezo huo dhidi ya Sudan ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa El Merreikh, Omdurman nchini Sudan lilifungwa na Nahodha Msaidizi, Erasto Nyoni na kuifanya mechi hiyo kumaliza kwa mabao 2-1. 

Fainali za CHAN zimepangwa kufanyika Februari mwakani nchini Cameroon.