Madai ya rushwa yaizindua CCM

22Oct 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Madai ya rushwa yaizindua CCM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na kuweka wazi madai ya kuwapo rushwa katika kura za maoni za uchaguzi wa serikali za mitaa, huku kikiwaonya wanaojihusisha na vitendo hivyo. 

Wakati kikitoa onyo hilo, chama hicho ambacho kinatawala nchi kwa sasa kimesema vitendo hivyo na madai ya upendeleo ni dalili za kupanga safu kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao wa Rais, wabunge na madiwani, utakaofanyika mwakani.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, alisema anatoa salamu za Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli, kuwa  amefurahishwa na uandikishaji unaoendelea na mwamko wa wananchi.

"Malalamiko tunayoyapokea yanagusa uvunjifu wa kanuni kwa mtazamo wa rushwa au upendeleo au kupanga safu. Upangaji wa safu mwingine nasikia wanadhani wanaweza kupanga kwa ajili ya uchaguzi. Mchezo huo tumeshauzuia na hatutauvumilia," alisema.

Dk. Bashiru alisema Mwenyekiti anawapongeza viongozi wa chama, wanachama na Watanzania kwa mwitikio mkubwa wakati wa uandikishaji na kwamba anaamini mwitikio utaendelea hadi wakati wa kupiga kura.

"Napenda kusisitiza haki itendeke, malalamiko tunayoyapokea yanavunja uvunjifu wa kanuni," alisema.Katibu mkuu huyo alisema kanuni za kuchuja wagombea hazikuzingatiwa kwenye baadhi ya maeneo na kwamba baadhi ya viongozi walichezea muhtasari kiasi cha kupishana kati ya tawi kata na uamuzi wa wilaya.

"Tunaelekeza maeneo hayo uchaguzi urudiwe, hakuna kuchukua fomu upya, hakuna mchujo bali wote walioomba wapigiwe kura. Kokote ambako uchaguzi utaporudiwa wagombea wote wataruhusiwa. Mfano wilaya za Kawe na Kinondoni wagombea watakuwa wote na si wale waliokwisha kuteuliwa," alisema.

Dk. Bashiru alisema wengi walikuwa wamepoteza imani na kwamba ili kurejesha imani wagombea watakuwa wote walioomba na kwamba maeneo kulikuwa na zogo na fujo, uchaguzi urudiwe bila kuwachuja wagombea.

Katibu Mkuu huyo alisema kulikuwa na rafu za kuchomoa majina kwenye masanduku ya kura na masanduku kubomolewa na wengine wakitumia jina la Katibu Mkuu kuwa amewapa maelekeo ya kufanya wafanyayo.

Alisema nyingine ni wasimamizi kuchelewa na kura za maoni zikaanza kupigwa baada ya saa tisa alasiri, na kwamba wagombea wote walioomba warudishwe kupigiwa kura.

"Marudio yanarekebisha uteuzi, kote uchaguzi urudiwe bila kuwachuja wapiga kura ili tweke imani, ilikuwa tumaliza Oktoba 29 tunaongeza siku mbili hadi Octoba 31, mwaka huu" alisema.

Alisema kwa mfano Mbeya kuna mgombea amempiga kibao mwenzake na kwamba wana CCM wanapaswa kuwa mfano bora na kuwa na uvumilivu hata wanapopishana kwa kutotumia lugha chafu au kuhamaki. "Tunahimiza kuwa Takukuru inakamata wala rushwa wakati wa uchaguzi na wakati usikio wa uchaguzi ndani ya CCM na nje, chombo hiki tumeunda sisi na moja ya ahadi zetu ni kupambana na rushw ana ufisadi," alisema.

Dk. Bashiru alisema chama kimeweka utaratibu wa kutoa taarifa kwenye chama na tuyo mwenye jukumu hilo, na kwamba anayezungumza atapaswa kutoa idhibni kwa msemaji mkubwa na kwamba hawataruhsiwa kutangaza matokeo kwa kuwa mchakato wa uchaguzi ni wa ndani. WAGOMA KUPIGA KURA

Wanachana wa CCM Tawi la Kasanga B, Kata ya Mindu, Morogoro Mjini, juzi waligoma kupiga kura za maoni kwa ajili ya kuchagua wanachama watakaogombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa baada ya kukosa mwafaka wa kusikilizwa madai yao. 

Madai ya wanachama hao  ni pamoja na kutaka uongozi wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini kuingilia kati na kurudisha majina ya  wagombea wote waliojitokeza katika kinyanganyiro hicho ili kufanya uamuzi wenyewe baada ya baadhi ya majina kukatwa na uongozi wa kata.

Sakata hilo lilianza juzi asubuhi  baada ya wanachama hao kujitokeza  katika viwanja vya CCM Kasanga B ili kushiriki kupiga kura za maoni, lakini ghafla walikuta baadhi ya wagombea majina yao hayapo na kuanza kwa mzozo huo. 

Mmoja wa wanachama hao, Juma Abdul, alisema baada ya kufika katika viwanja hivyo majira ya saa 2:00 asubuhi wakiwasubiri wasimamizi wa uchaguzi ambao walichelewa na hadi saa 7:00  mchana huku wanachama wakiwa wamekata tamaa na baadhi yao kuondoka. 

Alisema baada ya wasimamizi hao kufika, walianza kusoma majina ya wagombea huku wengine majina yao yakiwa hayapo ndipo ulipoanza mzozo huo na kutaka majina mengine yarudishwe ndipo kura zipigwe. 

Naye Amina Rashid alisema viongozi wa CCM wa kata hiyo wamefanya ujanja na kuweka majina wanayotaka ikiwamo kukata majina ya wanawake walioingia katika kinyang’anyiro hicho na kubakisha wanaume, hivyo hawako tayari kufanya uchaguzi mpaka uongozi wa wilaya ufike kutatua tatizo hilo.

Baada ya mzozo huo, Katibu wa CCM Kata ya Mindu, Hamisi Halili, alisema  wamerudisha majina hayo sita baada ya kufanya mchujo  ili wanachama wachague hatua ambayo ilipingwa vikali na kuamua kususia uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma, alikiri kutofanyika uchaguzi huo na kwamba tayari wameingilia kati mchakato huo ikiwa pamoja na kurudisha majina yote ya wagombea waliomba nafasi hiyo ili wanachama wafanye uamuzi wa kuchagua wale wanaowataka. Alisema walitarajia uchaguzi huo ufanyike jana.

DODOMA KURUDIWA 

KATIBU wa CCM Mkoa wa Dodoma, Janath Kayanda, ameagiza vituo vyote  ambavyo uchaguzi  haukufanyika, mchakato huo ufanyike leo. 

Kayanda alisema jana kuwa changamoto mbalimbali zilijitokeza na kukwamisha uchaguzi na kuagiza majina yote ya wanachama walioomba  nafasi ya uenyekiti ndani ya chama katika maeneo yao, yaingie kwenye utaratibu wa kupigiwa  kura  upya.

Kayanda alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchama wa CCM alipotembelea baadhi ya vituo ambavyo havikufanya uchaguzi katika Jiji la Dodoma jana kutokana na kuwapo kwa malalamiko mbalimbali kutoka kwa wanachama.

Aliagiza  marudio ya uchaguzi huo kusimamiwa kwa karibu na viongozi wa chama kuanzia ngazi ya tawi hadi wilaya ili kusikiliza malalamiko yanapojitokeza kwenye vituo vya kupigia kura.

Naye Selemani Issa, aliyekuwa mgombea katika nafasi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkwajuni Kata ya Kiwanja cha Ndege Wilaya ya Dodoma, alitaja changamoto zilizosababisha wanachama hao kukata rufani ofisi ya wilaya ni kutoridhishwa na utaratibu uliotumika kurudisha majina ya wagombea.

Aliitaja changamoto nyingine ni wagombea kutopewa nafasi ya kujinadi kwa wapiga kura kama utaratibu ulivyoelekeza kuwa kabla ya uchaguzi kufanyika lakini matokeo yake wanachama wamekutana na majina kwenye vituo vya kupigia kura bila kuwajua wahusika sura zao.

Pia alisema sababu nyingine ni kukatwa kwa baadhi ya majina ya wagombea ambao walichukua fomu kuomba kuchaguliwa kwa nafasi za wenyeviti na wajumbe wa mitaa husika.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma Dodoma, Robert Mwinje, alisema katika eneo lake kuna baadhi ya vituo katika kata zisizozidi 10 havikupiga kura kutokana na changamoto hizo zilizojitokeza.

Alizitaja baadhi ya kata ambazo vituo vyao hawakupiga kura kwa sababu ya malalamiko yaliyojitokeza kuwa ni Chang'ombe, Nkuhungu, Msalato, Dodoma Makulu, Kiwanja cha Ndege, Matumbulu na Hombolo.

Mwenyekiti huyo baada ya kutembelea kituo cha Njedengwa Magharibi aliagiza kurudiwa kwa uchaguzi katika kituo hicho jana mchana na wanachama wote walioomba kuchaguliwa, majina yao yaingie kwenye orodha ya wagombea. 

Imeandikwa na Mwandishi Wetu, DAR,  Ashton Balaigwa, MOROGORO na Ibrahim Joseph, DODOMA.

Habari Kubwa