Wakulima Mpwapwa wapewa somo tabianchi 

22Oct 2019
Peter Mkwavila
MPWAPWA
Nipashe
Wakulima Mpwapwa wapewa somo tabianchi 

WAKULIMA wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma wametakiwa  kuzingatia  ushauri wa kitaalamu ili kulima kilicho chenye tija na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Wito huo ulitolewa jana na Ofisa Kilimo na Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Maria Lesharu, alipokuwa akizungumza na wakulima wa kijiji cha Inzomvu Kata ya Kimagai wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mkulima yaliyoandaliwa na Chama cha Kilimo cha Mboga na Matunda (Taha).

Lesharu alisema ili kilimo kiwe na tija na wapate mazao mengi lazima wazingatie ushauri wa  wataalamu kutokana na ukanda wa mazao.

Aliwataka kutolima kilimo cha mazoea kwa kulima zao moja kila msimu jambo ambalo linasababisha wapate mavuno kidogo huku wakiwa wamepoteza nguvu nyingi.

"Tunapozungumzia  kufikia Tanzania ya viwanda, mkulima mdogo anahusika  moja kwa moja katika kuzalisha malighafi zitakazotumika viwandani. Tukiendelea kulima kwa mazoea hatutaweza kulifikia soko," alisema.

Ofisa huyo alisema ni muhimu wakaunganisha nguvu kwa kujiunga kwenye vikundi ili kufikia malengo makubwa.

Ofisa Miradi wa Taha,  Elianchea  Shang’a, alisema chama hicho kinajihusisha na kuendeleza kilimo cha mboga, matunda na maua  na kinalenga kumjengea uwezo mkulima mdogo kuondokana na  kilimo cha mazoea na kulima kilimo ambacho kitamsaidia kujikwamua na umaskini.

Alisema Taha inaboresha mazingira wezeshi ya biashara  ya mazao ya matunda,  mboga na maua  kwa kutoa ushauri na taarifa  za masoko kwa wakulima wadogo wa kati na wakubwa.

Naye mkulima wa matikiti maji wilayani Mpwapwa,  Aidan Ulaya,  alisema aliamua kulima zao hilo kwa lengo la kufanya mabadiliko ya kilimo na kuachana na kilimo cha mazoea.

Mkulima huyo aliiomba serikali kuongeza wataalamu wa kilimo vijijini na kuwekeza kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa ndich chenye tija.

Pamoja na kuchukua uamuzi huo, alisema  kuwa bado kuna na changamoto kubwa ya masoko ya mazao.

Pia alisema changamoto  kubwa inayowakabili wakulima wengi vijijini ni kukosa taarifa sahihi za masoko na kuuza mazao  yao kwa walanguzi ambao huwapunja wakulima.