Lukuvi ataka wananchi wasilipie zaidi ya 150,000 ardhi

22Oct 2019
Dotto Lameck
Tanga
Nipashe
Lukuvi ataka wananchi wasilipie zaidi ya 150,000 ardhi

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amewataka wananchi wanaoishi katika miji midogo na mikongwe wasilipe zaidi ya Sh 150,000/- kwa ajili ya kulipia ardhi ili kupata hati miliki.

William Lukuvi

Lukuvi amezungumza hayo katika program aliyoianzia ijulikanayo kama funguka kwa Waziri, uliofanyika wilayani Handeni mkoani Tanga kuhusu migogoro ya ardhi inayoendelea wilayani humo, huku akifafanua sheria ya ardhi ni kumilikiwa na mtu mmoja na sio wawili.

“Hatuwezi kuvumilia kuona ardhi inagombaniwa na watu wawili, sheria hairuhusu hivyo ni lazima abaki mmoja na atakaye sababisha sahara hiyo atakuwa amefanya chini ya Halmashauri, hivyo Halmashauri italazimika kuchukua gharama ya kumtafutia huyo mwingine kiwanja kingine” Amesema Lukuvi

Lukuvi amemuagiza Bwana Ardhi na Kamishna wa kanda yake kufanya upekuzi wa mashamba yaliyopo Handeni ili kuona kama yanaendelezwa na kuleta tija, na kuwataka wamiliki wa mashamba ambao hawana kazi nayo kwa muda huo wayarudishe kwa serikali.

“Kazi ya kuweka akiba ya ardhi ni kazi ya serikali, kuna watu wamepewa mashamba hapa handeni hawajaendeleza kwa miaka mingi lakini hati zao zipo banki wamekopa pesa na kwenda kujenga sehemu nyingine sio hapa handeni, kama ni shamba la mifugo tulikute kweli linafuga kisasa, na kama ni shamba la kilimo tunataka tuwe tunapima uendelezaji ili tuone vijana wanaajiriwa pale”Amesema.

Aidha, Lukuvi amewataka Mameneja wa mabenki kuhakikisha wanasimamia watu wanaokopa pesa kwa kuweka dhamana ardhi kuwa fedha hizo zinarudi katika eneo husika kama hati ya ardhi inavoeleza lasivyo ardhi hiyo itachukuliwa na serikali hali ambayo iyawapelekea kupata hasara.

Habari Kubwa