Wadau wachambua rushwa uchaguzi mitaa

23Oct 2019
Mary Geofrey
Nipashe
Wadau wachambua rushwa uchaguzi mitaa

BAADHI ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamepongeza uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchukua hatua dhidi ya rafu, rushwa na figisu figisu zilizojitokeza kwenye kura za maoni za uchaguzi wa serikali za mitaa ndani ya chama hicho.

Kura za maoni zilifanyika mwishoni mwa wiki kuteua wagombea watakaopeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo wa Oktoba 24, mwaka huu.

Mratibu wa Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema lipo tatizo la watu kuamini kuwa kwenye siasa au wakati wa uchaguzi ndiyo wakati wa kuvuna fedha.

“Ni jambo jema kama CCM imeona hili na kuchukua hatua, ni hatua nzuri kuwa wameona mambo hayako sawa wanachukua hatua,” alisema na kuongeza:

“Tatizo la watu wengi ni kufanya siasa kuwa sehemu ya kupata hela kutumia fedha au kutoa rushwa bado halijaondoka.”

Alisema kumekuwa na historia ya muda mrefu kuwa wakati wa uchaguzi ndiyo wakati wa kuvuna na kwa chama kama hicho kutoa karipio kutawaweka watu sawa na kurudi kwenye mstari.

“Tunampongeza sana Dk. Bashiru kwa kukemea na kuchukua hatua, ameonyesha kuwa kipindi cha uchaguzi siyo kipindi cha kuvuna fedha au kutoa rushwa bali kuchagua viongozi sahihi,” alisema Olengurumwa.

Mchambuzi wa masuala ya Siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Alex Benson, alisema zinaashiria kuwa bado jamii haina uelewa kuhusu maana ya dhamana.

Alisema vitendo hivyo vinaashiria kuwa bado watu wana tamaa ya madaraka kwa manufaa binafsi na siyo wanataka kuwania kwa lengo la kuhudumia jamii.

Benson aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, kuhusu malalamiko ya kuvunjwa kwa kanuni na mtizamo wa rushwa, upendeleo na kupanga safu kwa ajili ya uchaguzi ujao wa mwaka 2020 na maamuzi yaliyochukuliwa na CCM, yaliyoibuka kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho.

“Kinachotokea katika siasa za Tanzania ni ukosefu wa maadili ya uongozi, bado watu au wanachama wa vyama hawafahamu nini maana ya uongozi, ndio sababu ya kutumia fursa hizo kuwania kwa lengo la kujikwamua kimaisha,” alisema Benson.

Alisema taratibu zipo na kila sehemu na zinazofahamika, lakini kama ikitokea watu wakaendelea kukengeuka inamaanisha kuna ukiukwaji wa maadili ndani ya chama au ndani ya jamii.

“Ninavyoona haya yote yanatupa taswira ndani ya jamii yetu kuwa bado watu hawajawa na uelewa wa namna ya taratibu za kumpata kiongozi ziko sahihi zibadilishwe au kama hazifai,” alisema.

Alisema kizazi hiki ni cha kuhoji wenye mamlaka, hivyo yanapotokea mambo kama hayo yanaleta taswira ambazo zina tafsiri mbalimbali.

Alisema kinachotakiwa ni elimu kutolewa ndani ya vyama na nje kwa lengo la kujenga uelewa mpana wa namna ya kukabiliana na changamoto hizo.

Kutokana na kuwapo kwa rafu hizo, juzi Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, akitoa salamu za mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli, aliagiza uchaguzi urudiwe bila wagombea kuchukua tena fomu na wagombea wote watapigiwa kura badala ya kupitishwa kwenye kura za maoni.

“Tunaelekeza maeneo hayo ya uchaguzi urudiwe, hakuna kuchukua fomu upya, hakuna mchujo bali wote walioomba wapigiwe kura. Kokote ambako uchaguzi utarudiwa wagombea wote wataruhusiwa mfano wilaya za Kawe na Kinondoni wagombea watakuwa wote na si wale waliokwishateuliwa,” alisema Dk. Bashiru.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafuatiwa na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika mwakani.